MBOWE: TUNAWAFAHAMU WOTE WANAOTAKA KUHAMA CHADEMA


Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema wanawafahamu Wanachama wote wa chama hicho wenye nia ya kutengeneza migogoro na baadaye kuhama.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Chadema amesema hawawezi kuwafukuza katika chama hicho hadi pale watakapoamua kuondoka wenyewe.

Mbowe aliyasema hayo jana alipohojiwa kuhusu makada wa Chadema waliokihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi hivi karibuni.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alidai makada wa chama hicho waliotimkia CCM hivi karibuni, ni majeruhi wa uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana na baadhi yao kushindwa kutetea nafasi zao

“Tunatambua watu ambao wanatengenezwa ili wazue migogoro ndani ya chama chetu, na tunatambua watu ambao wakati wowote wakikamilisha malengo waliyopewa, wataondoka.

“Hatuwezi kuwafukuza kwa sababu hata tukiwafukuza, baadaye watapiga kelele tumefukuzwa... tumefukuzwa... tumeonewa... tumeonewa! Tunawaacha waondoke wenyewe kwa utashi wao," alisema.

Alisema sababu zinazotolewa na makada hao kwa sasa hazina mashiko kwa kuwa chama kinatambua kuondoka kwao kunasukumwa na matokeo ya majeraha waliyoyapata katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho na si rahisi kuwazuia.

“Wote hao walipoingia, walitoa kauli nzito nzito, lakini katika kipindi cha miaka mitatu, minne, wanatoka wanakimbia sasa. Leo wakitoka wanapiga kelele, haiwasaidii," alisema.

Mwanzoni mwa wiki, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji, alikihama Chadema na kujiunga na CCM, akidai chama hicho kikuu cha upinzani nchini hakina uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi na kimekuwa na malumbano na migogoro ya ndani.

Dk. Mashinji alitangaza uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chadema katika uchaguzi uliopita, Cecil Mwambe, kutangaza mwishoni mwa wiki kujiuzulu ubunge wa Ndanda na uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM.

Vigogo wengine walioihama Chadema na kurejea CCM walikotoka ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Credit: Nipashe


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post