MADALALI NA WAENDESHA MINADA WASIOFUATA SHERIA KUKIONA CHA MOTO

Na Ramadhani Kissimba, WFM, Dar Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James mewaonya madadali na waendesha minada Tanzania Bara kuacha mara moja kufanya biashara hiyo bila kujisajili kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Bw. James ametoa onyo hilo Jijini Dar es Salaam wakati akizundua Mfumo Mpya wa Kieletroniki wa utoaji leseni za udalali na uendeshaji wa minada ya hadhara Tanzania Bara ambapo watoa huduma hiyo kuanza sasa wanatakiwa kujisajili kupitia mfumo huo kwa njia ya mtandao wa Internet ama kupitia simu zao za kiganjani.

‘’Napenda kuwafikishia taarifa hii wananchi wote, hasa Madalali na waendesha minada, kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kufuatilia na kuchukua hatua kali kwa wote watakaojuhusisha na shughuli za udalali na uendeshaji wa minada bila kuwa na leseni halali’’ alisema Bw. James.

Aliziagiza Taasisi zote za Serikali kufanya kazi na Madalali na waendesha minada ambao wanatambulika kisheria na kwa kufanya hivyo watakuwa wameisaidia Serikali kujipatia mapato yatakayotokana na ada ya leseni itakayolipwa na wafanyabiashara ya udali na waendesha minada.

“Mfumo huu utapunguza changamoto zilizokuwepo hapo awali ambazo zilikuwa zinatumia mlolongo mrefu wa kupata leseni kwa kuwa mfumo huo  umeunganishwa na Mfumo wa Malipo wa GePG ambapo mwombaji ataweza kulipia ada ya leseni kwa kutumia benki, mawakala au simu za kiganjani na hivyo kurahisisha na kuboresha ulipaji, kupunguza gharama za ulipaji na kuongeza uwazi na udhibiti wa Fedha za Umma.

Bw. James aliutangazia Umma kuwa kuanzia  tarehe 24 Februari, 2020 maombi yote ya leseni za Udalali na Uendeshaji wa Minada Tanzania Bara yawasilishwe kupitia Mfumo wa Utoaji wa Leseni za Udalali na Uendeshaji Minada ambao unapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango (www.mof.go.tz);

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Bw. Chotto Sendo, amesema biashara ya udalali na uendeshaji wa minada hapa nchini imekuwa ikikua kwa kasi na hivyo kutengeneza ajira, kuongeza kipato pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Bw. Chotto aliongeza kuwa leseni za Udalali na uendeshaji wa minada Tanzania Bara zinatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa mujibu wa sheria ya waendesha minada ya Mwaka 1928 iliyorejewa Mwaka 2002, na Wizara imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kutatua changamoto zinazowakabili wadau hawa ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Wakizungumza kwa niaba ya madalali, Mwenyekiti wa Chama cha Mdalali wa Mahakama Bi. Mwamvua Kigulu na Mwenyekiti wa madalali Binafsi Bw. Phidel Katundu, wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kubuni mfumo huo utakao wapunguzia gharama ya kufuata huduma ya usajili jijini Dodoma.

Wameiomba Serikali kudhibiti madalali wasio na leseni au wale wasiosajiliwa kwa kuwa wanaikosesha Serikali mapato pamoja na kuchafua taswira ya biashara ya udalali nchini.

Wamemwomba Katibu Mkuu Bw. Doto James kupitia upya Sheria ya Udalali ya Mwaka 1928 ambayo wamesema imepitwa na wakati na inakwaza shughuli za udalali nchini ikiwemo urasimu wa ufanyakazi kazi zao kutoka kwa mamlaka za Serikali Kuu hasa makatibu Tawala wa Wilaya ambao wanataka kupata vibali kutoka kwao kabla ya kutekeleza kazi zao za udalali katika maeneo husika.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527