WANAUME WAHOFIA WAKE ZAO KUROGWA WAKIGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI


Mjumbe wa Baraza la Wanawake CCM (UWT) wilaya ya Meatu, Avelina Mwigulu akizungumza wakati wa warsha ya ufuatiliaji wa kazi za uhamasishaji wa jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi na michakato ya maamuzi na uongozi iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kukutanisha pamoja wadau kutoka makundi ya viongozi wa mila,dini na jamii kutoka mikoa ya Shinyanga (Kishapu),Kigoma (Kasulu), Tabora (Uyui), Mara (Tarime) na Simiyu (Meatu) lengo likiwa ni kuongeza nafasi za wanawake katika nafasi za uongozi. Alisema wanaume wenye hofu ya Mungu wanapata hofu kuwaruhusu wake zao kujihusisha na masuala ya siasa kwamba watajihusisha na masuala ya ushirikina. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), wilaya ya Meatu Elizabeth Kabati akizungumza katika warsha hiyo ambapo alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakishindwa kugombea nafasi za uongozi kwa hofu ya familia zao kurogwa.
Mjumbe wa Kitengo cha wanawake katika Chama cha Walimu wilaya ya Meatu,Christina Paga akiwasilisha matokeo ya kazi za uhamasishaji wa jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi na michakato ya maamuzi na uongozi zilizofanywa na wadau mkoani Simiyu. Aliitaka jamii kuacha kuhusisha uongozi wa mwanamke na imani za kishirikina.
Katibu Kinyaki Teachers SACCOS Meatu Rahel Silvester akizungumza katika warsha hiyo ambapo aliwataka wanawake kujiamini na kutokata tamaa ili kufanikiwa kushika nafasi za uongozi katika jamii.
Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa nguvu za pamoja (TAPO) TGNP Grace Kisetu akizungumza wakati wa warsha ya ufuatiliaji wa kazi za uhamasishaji wa jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi na michakato ya maamuzi na uongozi.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 
Imeelezwa kuwa baadhi ya wanaume wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wanaogopa kuwaruhusu wake zao kugombea nafasi za uongozi ikiwemo siasa wakihofia kuwa watajihusisha na masuala ya imani za kishirikina.

Hayo yamebainishwa na wadau wa haki za wanawake kutoka mkoa wa Simiyu katika Warsha ya ufuatiliaji wa kazi za uhamasishaji wa jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi na michakato ya maamuzi na uongozi iliyofanyika Jumapili Februari 16,2020 katika Ukumbi wa Vijana Center Mjini Shinyanga.

Mjumbe wa Baraza la Wanawake CCM (UWT) wilaya ya Meatu, Avelina Mwigulu alisema wanaume wenye hofu ya Mungu wanapata hofu kuwaruhusu wake zao kujihusisha na masuala ya siasa kwamba watajihusisha na masuala ya ushirikina.

“Baadhi ya wanaume wana imani potofu kuwa mtu yeyote anayetaka kuwa kiongozi lazima aende kwa mganga wa kienyeji, hivyo wanasema mama anapoanza kuchukua fomu kugombea,lazima aende kwa waganga akagangwe ndiyo maana wanaume wenye hofu ya Mungu wanahisi wake zao watajihusisha na vitendo vya ushirikina”,alisema Mwigulu.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), wilaya ya Meatu Elizabeth Kabati alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakishindwa kugombea nafasi za uongozi kwa hofu ya familia zao kurogwa.

“Jamii bado inaamini kuwa endapo unataka kugombea nafasi ya uongozi lazima uende kwa mganga wa kienyeji ili mambo yako yawe sawa. Baadhi ya wanaume wanapata hofu kuwa wake zao na familia zao zitaandamwa kurogwa na hivyo kusababisha familia iingie kwenye matatizo matokeo yake familia zitajihusisha na vitendo vya kishirikina”,aliongeza Kabati.

“Tunaendelea kuielimisha jamii kuwa Uongozi siyo lazima kushika dawa bali kinachotakiwa ni Kumwamini Mungu na kuishirikisha familia na jamii ikukubali,jamii ikukubali lazima itakuunga mkono na utafanikiwa kuwa kiongozi katika jamii”,alisema Kabati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa VIKOBA kata ya Mwamishali wilaya ya Meatu,Enock John alisema ni kweli kuna baadhi ya wanaume wana imani potofu wanasema haiwezekani mtu kusimama mwenyewe akajiamini na kuwa na ujasiri bila kushika dawa katika uongozi wa kisiasa.

Aliwataka wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kuwa na nguvu ya ushawishi katika jamii huku akieleza kuwa ili ufanikiwe unatakiwa kumjua Mungu kwani mtu mwenye hofu ya Mungu ana maadili mema.

“Wanawake ni jeshi kubwa,mwanamke ni kiongozi tangu kuzaliwa kwake hata katika familia mwanamke ndiyo nguzo kuu,kutokana na uwezo wake anatakiwa kuwa kiongozi ili kusaidia kuleta maendeleo yenye tija katika jamii”,aliongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527