Na Anitha Jonas – WHUSM
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Hassan Abbasi amesema kuwa wizara haitaingia mkataba na mtoa huduma yoyote wa sekta binafsi ambaye hajasaini kiapo cha uadilifu na BRELA.
Dkt.Abbasi ametoa tamko hilo jana Jijini Dodoma, alipokuwa akifanya kikao na wafanyakazi wa Wizara mara baada ya kuapishwa kwa lengo la kuzungumza na wafanyakazi na kutoa maelekezo ya utekelezaji wa majukumu ambapo amesisitiza kuwa sekta zote za wizara ni nguvu laini ya nchi (soft power).
“Katika semina hii ya kiapo cha uadilifu tumejifunza kuwa watoa huduma wote kutoka sekta binafsi wanapokuwa wanaingia mikataba na serikali wanapaswa wawe wamesaini kiapo cha uadilifu na BRELA pia waweke uthibitisho wa kiapo hicho kwenye mkataba na katika kusimamia kiapo hichi nasisitiza uadilifu kwa watumishi,uzalendo na uwajibikaji," alisema Dkt.Abbasi.
Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo wa wafanyakazi Katibu Mkuu huyo alisisitiza mambo mbalimbali kwa wafanyakazi ikiwemo umuhimu wa kuchapa kazi kwa kuzingatia muda pamoja na kuacha majungu kazini na ugoigoi.
Naye Kaimu Katibu Msaidizi Sekretariaeti ya Maadili kwa Umma Kanda ya Kati Bibi. Bibi.Jasmine Bakari alifafanua kuwa utaratibu wa kiapo cha ahadi ya uadilifu hufanyika katika vipindi mbalimbali ikiwemo pale kiongozi anapobadilishwa, hivyo watumishi hutakiwa kutoa ahadi ya kiapo cha uadilifu kwa kiongozi huyo.
“Semina tuliyotoa leo katika wizara hii ni sehemu ya majukumu ya taasisi yetu na tumekuwa tukifanya hivi kwa lengo la kuwakumbusha watumishi wa umma kuhusu kiapo cha uadilifu katika utendaji”. Alisema Bibi.Jasmine.
Halikadhalika nae mmoja wa wafanyakazi wa Wizara hiyo kutoka Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani Bi.Happiness Kalokola alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kikao alichokifanya pamoja na mafunzo yaliyotolewa kwani yamesaidia kuwakumbusha watumishi suala la uadilifu.