WANANCHI SHINYANGA MJINI WAGOMBANIA NYAMA YA FISI MWENYE HIRIZI...SHUHUDIA HAPA

Mwananchi akikata mguu wa fisi huyo


Katika hali isiyo ya kawaida wakazi wa kata ya Ngokolo Mjini Shinyanga wamegombania nyama ya fisi waliyemuua baada ya kuonekana akiranda randa katika kata hiyo. 

Tukio hilo la aina yake limetokea leo Ijumaa Februari 7,2020 majira ya mbili usiku katika mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo ambapo mamia ya wananchi wameonekana wakisukumana huku wengine wakikata viungo vya mnyama fisi anayedaiwa kuwa na hirizi katika mguu wake wa mbele. 

“Huyu fisi ametokea maeneo ya Seif Hotel,akaelekea maeneo ya Stendi ya mabasi Mjini Shinyanga,wananchi wamemkurupusha Stend,akatokezea eneo la Mapinduzi shule ya Msingi,kisha Mshikamano baadae akaingia kwenye kalavati/daraja lililopo mtaa wa Magadula karibu na barabara ya Mohamed Trans. 

“Huyo fisi alivyoingia kwenye kalavati akatulia humo,wananchi wakachoma tairi upande wa pili,kutokana na moshi fisi akatoka, ndipo mmoja wa wananchi hao akampiga jiwe huyo fisi akaanguka. Jamaa aliyempiga jiwe akakata mguu wa mbele wenye hirizi,akaondoka zake na wananchi wakaendelea kugombania viuongo vya fifi,kila mmoja akikakata kiungo alichoona kinamfaa. Askari polisi wamefika ikashindikana kuondoa wananchi",Mashuhuda wameiambia Malunde 1 blog.

Tukio hili limehusishwa na imani za kishirikina kutokana na madai kwamba fisi huyo alikuwa na hirizi na siyo rahisi fisi kuonekana mjini kwani fisi mara nyingi hupendelea kwenye mapori/vichaka.

Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa baada ya fisi huyo kuuawa na wananchi kugawana nyama,mwanamke mmoja ameonekana eneo alipouawa fisi huyo na kuanza kuangua kilio akidai fisi wake kauawa.

"Yaani huku ni vituko,kuna mama kaja mpaka eneo alipochinjiwa fisi akaangua kilio fisi wake wamemchinja akaanza kutafuta kichwa hajakipata,akawaambia watu fisi wangu alikuwa na kitu bora wangenirudishia tu. Kazoa mabaki yote kaondoka nayo alikuwa na bodaboda. Watu walivyoona hivyo wamemfuata na daladala na bodaboda kwa nyuma hadi wajue anakoelekea",amesema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Tazama video hapa chini



Tazama hapa chini picha wananchi wakigawana nyama ya fisi










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527