RC TELACK : MWAKA HUU TUNAINGIA MIKATABA YA KAZI NA WALIMU


Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa Mhe. Zainab Telack, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama Annamringi Macha na kulia ni Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza na Maafisa Elimu kata, Watendaji wa kata na Wakuu wa shule za msingi na sekondari(hawapo pichani) wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu, ambaye ni Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Bw. Mohamed Kahundi akitoa mwongozo wa Wizara ya Elimu kuhusu upangaji wa vipindi shuleni katika kikao hicho
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa katika kikao hicho
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akiwa darasani katika shule ya msingi Ukune, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu akifuatilia ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi, kulia ni Katibu Tawala Mkoa Bw. Albert Msovela
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akiagiza kukarabatiwa kwa viti na meza katika shule ya sekondari Ukune, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu 
***
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amesema mwaka huu 2020 ataingia mkataba wa kazi na Waratibu wa Elimu kata ili kuweka mikakati ya kuhakikisha ufaulu mzuri katika mitihani ya Taifa ya darasa la saba na kidato cha nne.

Akizungumza katika kikao cha pamoja na Watendaji wa kata, Waratibu Elimu kata na Wakuu wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Wilaya ya Kahama jana tarehe 31/01/2020, Mhe. Telack amesema lengo la mikataba ni kuhakikisha kuwa kila mmoja anasimamia Elimu kikamilifu kwenye eneo lake ili kuongeza ufaulu.

"Mimi mwenyewe nitasaini Mikataba moja kwa moja na Waratibu Elimu kata nao watasaini na Wakuu wa shule pamoja na walimu, nataka kuona watoto wanatoka darasa la kwanza wanajua kusoma na kuandika, mjipangie mikakati ya kuondoa sifuri" amesema Telack.

Ili kufanikisha mkakati huo, Mhe. Telack amewataka Waratibu wa Elimu kata kuwasilisha kila mwezi taarifa ya maendeleo ya taaluma kwenye kila shule.

Aidha, amesema kuwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu kila baada ya miezi miwili ifanyike mitihani ya kuwapima wanafunzi ili kubaini changamoto na kuzifanyia kazi.

Amesisitiza pia ni lazima kuhakikisha mitaala inakamilishwa ili wanafunzi wapate nafasi ya kufanya marudio kabla ya mtihani.

Telack amekemea tabia ya baadhi ya walimu kuwaachia wanafunzi kujisimamia ikiwemo kufuatlia mahudhurio yao wakati walimu wa madarasa wapo. "Walimu tumefikia pabaya, walimu wa madarasa hawafanyi kazi yao, sitaki kusikia"

Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Elimu ambaye ni Afisa Elimu Mkoa, Bw. Mohamed Kahundi amewataka wasimamizi wote Elimu Mkoani hapa kufuata miongozo na maelekezo ya Wizara ya Elimu katika kuandaa ratiba za vipindi ili kukamilisha mitaala.

"Tusibadilishe miongozo na melekezo ya Wizara katika kuandaa vipindi" ,amesema Kahundi.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewapa siku tatu Wakuu wote wa shule za msingi na sekondari Mkoani hapa kukarabati madawati, viti na meza kwa fedha ya ukarabati inayoletwa na Serikali kila mwezi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post