WAZIRI MKUU: SERIKALI HAIWEZI KUFUTA UCHAGUZI WOTE WA SERIKALI ZA MITAA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema licha ya kuwepo kwa ugatuaji wa madaraka (D by D), Serikali za Mitaa bado zina wajibu wa kuwahudumia wananchi kwa sababu ziko karibu nao zaidi kuliko Serikali Kuu.

Ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Januari 30, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Bi. Ruth Mollel, kwenye kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni. Mbunge huyo alisema dhana ya ugatuaji wa madaraka inakinzana na hali halisi kwani utekelezaji wake haujaenda sawasawa kwa vile Serikali inakusanya fedha kutoka kwenye vyanzo vya mapato vya Halmashauri kama vile kodi ya majengo na mabango.

“Wajibu wa kumhudumia mwananchi ni wa Serikali za Mitaa kwa sababu iko karibu nao zaidi. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kuwa tunashirikiana na Serikali za Mitaa kumhudumia mwananchi lakini hatujaondoa wajibu wa Serikali za Mitaa kuwahudumia wananchi,” amesisitiza.

Amesema Serikali Kuu bado inalo jukumu la kusimamia mapato na imeamua kudhibiti ukusanyaji wa mapato na imekuwa ikihakikisha mapato haya yarudi tena kwa wananchi. “Tunaporudisha kwa wananchi, tunawapelekea hao hao Serikali ya Mitaa kwa mahitaji yao ili watekeleze hilo jambo, hatujawaondolea mamlaka ya kusema tunahitaji darasa, tunahitaji kituo cha afya, tunahitaji uboreshaji wa miundombinu.”

“Tumeongeza hata taasisi kwa kuunda TARURA ili isimamie miundombinu; sasa hivi tunaenda kwenye maji, kutakuwa na taasisi ya kusimamia utoaji wa maji. Pale ambapo kuna mahitaji, Mamlaka ya Serikali za Mitaa iseme inahitaji shilingi ngapi, kwa ajili ya nini, nasi tunawapelekea, ndiyo kwa sababu leo tunaona huduma zinatekelezwa mpaka vijijini. Hii ni kwa sababu tunashirikiana na Serikali za Mitaa katika kuratibu.”

“Ule udhaifu wa usimamizi wa makusanyo, na udhaifu wa usimamizi wa matumizi ambao ulikuwa umejitokeza sasa tunaendelea kuutibu na ndiyo kwa sababu unaona wakati wote tunapokwenda huko kwenye ziara, kwanza tunauliza ukusanyaji na kama makusanyo yoyote yamehifadhiwa na matumizi yake yako sawa, na pale ambapo matumizi yanakuwa si sahihi tunachukua hatua,” amesema.

Amesema kutokana na muundo uliopo, zipo Serikali za Mitaa ambazo zina majukumu yake yaliyoainishwa rasmi na kuna Serikali Kuu ambayo pia inawajibika kuzihudumia Serikali za Mitaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema haitaleta maana endapo Serikali italazimika kutengua matokeo ya uchaguzi wote wa Serikali za Mitaa wakati wagombea ambao hawakuridhishwa na matokeo hayo walikuwa na fursa ya kukata rufaa.

“Chaguzi zote nchini zinatawaliwa na kanuni na sheria zake. Kila mmoja aliyeshiriki kama aliona kuna ukiukwaji wowote, alikuwa na fursa ya kukata rufaa na kama hajaridhika, alikuwa na fursa ya kwenda mahakamani,” alisema.

Alisema chaguzi zote zina sheria zake na kanuni zake na hata wakati wa kuandaa kanuni za Serikali za Mitaa, vyama vyote vya siasa vilishirikishwa katika kutengeneza kanuni zao na moja kati ya kanuni hizo ni pale ambapo inatoa fursa kwa yeyote ambaye hajaridhika huko anakogombea, anaweza kukata rufaa na atakapoona rufaa hiyo kwenye ngazi inayofuata haikutenda haki, aende mahakamani.

“Kwa hiyo kulichukua hili kwa ujumla ujumla, inaweza isiwe sahihi sana kwa sababu kila mmoja kule alipo, alikuwa na mamlaka yake inayoratibu na anayo fursa ya kwenda kwenye mamlaka kukatia rufaa pale ambapo hajaridhika na utekelezaji wa jambo hilo. Na vyama vyote vilishiriki kwenye hii kanuni ya kukata rufaa, kwa hiyo ni wajibu wa huyo mgombea kwenye eneo hilo kwenda kukata rufaa,” alisema.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Mbozi, Bw. Pascal Haonga, aliyetaka kujua kama Serikali iko tayari kurudia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu kwa sababu ule uliopita uligubikwa na dosari nyingi.

“Mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, uligubikwa na dosari nyingi sana zikiwemo za wagombea kutoka vyama vya upinzani kunyimwa fomu, ofisi kufungwa kwa muda wote, hivyo kupelekea baadhi ya wagombea hasa wa upinzani kushindwa kupata fursa za kugombea. Serikali haioni kwamba ni vema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uweze kurudiwa sambamba na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu?” alihoji.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post