MADINI NA VIWANDA VYALETA MAGEUZI YA UCHUMI NCHINI

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO

Mauzo ya bidhaa nje ya nchi zisizo kuwa za kawaida yameongezeka kwa asilimia 41.9 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwezi  Novemba, mwaka jana.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dodoma  na Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari .

Dkt. Abbasi amesema kuwa kupitia jitihada mbalimbali zinazochagizwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli zimesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuongeza mauzo ya bidhaa muhimu kwenda nje na ukuaji wa viwanda nchini  ikiwa ni sehemu muhimu ya  mageuzi ya uchumi nchini.

 “Wote mnafahamu kuwa Serikali imechukua hatua kubwa kuanzisha masoko ya madini na kuzuia uuzaji holela na utoroshaji wa madini. Matokeo yake tumeanza kufaidi. Hadi Novemba, 2019, mauzo ya dhahabu nje ambayo ni asilimia 51.4 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi yaani bidhaa zisizo za kawaida, yaliongezeka kwa asilimia 41.9 kufikia kiasi cha Dola Bilioni 2.1”, alisema Dkt. Abbasi

Aidha, aliongeza kuwa  “sera ya kuchagiza ujenzi wa viwanda nayo imezidi kulipa, ambapo  mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi  yameongezeka kwa asilimia 28.4 kufikia Dola milioni 996.0 ikichangiwa zaidi na bidhaa za chuma na mabati, vioo, tumbaku, katani na mbolea. 

Jitihada hizo za Serikali zimeendelea kusaidia kuongeza ajira kwa watanzania, sambamba na kuwa vyanzo vipya vya mapato huku vikitazamiwa kusaida uboreshaji wa huduma za kijamii.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post