TANZANIA YAWATAKA WANAFUNZI WANAOSOMA CHINA WASIRUDI KWANZA HUKO CHINA HADI WATAKAPOPEWA TAARIFA RASMI YA SERIKALI KUHUSU VIRUSI VYA CORONA


Serikali imewataka wanafunzi wanaosoma nchini China ambao wako likizo nchini Tanzania, kutorudi nchini humo kwanza hadi pale zitakapopatikana taarifa za kidiplomasia kuhusiana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona kwani Wizara ya Mambo ya Nje inaendelea kufanya mawasiliano na balozi zote mbili juu ya mwenendo wa ugonjwa huo.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Januari 30, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.

Amesema serikali itakaporidhika na hali inayoendelea nchini China itatoa tamko kwa Watanzania walioko likizo kurudi kuendelea na masomo na kwamba iwapo hali ikiendelea kuwa mbaya sana itatafuta utaratibu mwingine.

“Tunatambua kuna wazazi wana watoto wetu wanasoma nchini China na wengine wamesharudi likizo, tunawasihi watoto hao wasiende kwanza nchini China hadi tutakapopata taarifa za kidiplomasia.

“Wizara ya Mambo ya Nje Tanzania inaendelea kufanya mawasiliano na balozi zote mbili za China nchini Tanzania na Balozi ya Tanzania nchini China kuona mwenendo wa ugonjwa huo pale serikali itaridhika kwamba kule hali imepungua tutatoa tamko kwa Watanzania walioko likizo hapa nchini kurudi kuendelea na masomo na vinginevyo ikiendelea sana basi serikali itatafuta utaratibu mwingine,” amesema Majaliwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post