TUZO ZA DIJITALI ZAZINDULIWA TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Alhamisi, 16 Januari 2020,Dar es Salaam
Kwa mara ya kwanza, Tuzo za Dijitali (Tanzania Digital Awardszimeanzishwa nchini Tanzania. Tuzo hizi zinalenga kutambua na kutuza ubunifu, uvumbuzi na ufanisi katika kutumia teknolojia za kidijitali kwa minajili ya kuleta mabadiliko chanya ndani ya jamii ya Tanzania.

Tanzania Digital Awards ni kwa ajili ya watu binafsi, mashirika na taasisi ambazo zinatumia teknolojia ya kidijitali kibunifu, kivumbuzi na kiufanisi kwa lengo la kuhamasisha, kuleta mabadiliko na kuchagiza matokeo chanya na ya kudumu katika jamii. 

Mkuu wa Programu, Utafiti na Uvumbuzi wa Serengeti Bytes, Ndugu Genos Martin anasema tuzo hizi zinalenga kuwatambua wale wote ambao mchango wao unadhihirika kuwa bora katika matumizi ya mtandao na utoaji huduma.

"Tunataka kuwatambua watu binafsi, mashirika na taasisi ambazo zinatumia mitandao kuwasiliana na kutoa huduma katika namna bora na bunifu. Tuzo hizi ni za kipekee kwa kutambua na kutuza juhudi za kidigitali nchini. Tunakusudia kuifanya TDA kuwa tuzo za fahari zaidi nchini. 

Tunatazamia kuunga mkono na kuchochea juhudi zinazofanyika kuleta matokeo chanya katika mitandao ili kuleta tija katika biashara, siasa, burudani, utamaduni na jamii kwa ujumla. Tuzo hizi zinawakilisha kilele cha mapinduzi ya nne na ya tano ya viwanda nchini’’, anasema

Tanzania Digital Awards zinalenga kuchagiza Uwajibikaji, Ubunifu na Uvumbuzi kwenye Dijitali. Zikiwa katika Makundi tisa na zaidi ya vipengele vidogo 50, tuzo hizi ni za kwanza na kubwa zaidi kutambua juhudi zinazofanyika ili kuleta mapinduzi ya kidigitali Tanzania na nje ya mipaka.

Makundi ya tuzo ni pamoja na Serikali Mtandaoni, Maendeleo na Diplomasia Mtandaoni, Masoko Mtandao, Burudani Mtandaoni, Vyombo vya Habari Mtandaoni, Uvumbuzi wa Kidijitali, Mawasiliano ya Kidijitali, Uchechemuzi Mtandaoni na Tuzo ya Ujumla ya Chaguo la Watu. 

Mapendekezo ya wawania tuzo pamoja na mchakato wa kupiga kura vitafanyika kati ya tarehe 15 Januari hadi 15 Februari. Wahusika wanaweza kupendekezwa au kujipendekeza wenyewe.
Kupendekeza, tembelea www.digitalawards.co.tz 

Kwa Mawasiliano
Tutumie barua pepe: hello@serengetibytes.com
Wasiliana na Kennedy Mmari 
Simu Na. 0719 579 733
Tanzania Digital Awards imeletwa kwenu na Serengeti Bytes

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527