TFRA YAMKERA WAZIRI HASUNGA, ATAKA BEI YA MBOLEA ISHUKE

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Songwe
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha kuwa inapanga na kusimamia bei elekezi za mbolea kwa lengo la kumuwezesha mkulima kupata mbolea kwa bei nafuu.


Amesema kuwa bei ya sasa ya mbolea ya kukuzia na kupandia bado sio rafiki kwa wakulima hivyo TFRA wana wajibu wa kuhakikisha kuwa bei inapungua Zaidi.

Waziri Hasunga ameyasema hayo tarehe 21 Januari 2020 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha vyama vya ushirika kuhusu ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) kilichofanyika katika ukumbi wa Mpendejirani eneo la Vwawa Mkoani Songwe.

Amesema kuwa Kanuni za usimamizi na uagizaji wa mbolea kwa pamoja zilitungwa kufuatia tafiti za kina zilizofanywa na Watafiti wa ndani ya Nchi na wengine kutoka Taasisi za Kimataifa ambapo Matokeo ya Tafiti hizo yalionesha kuwa BPS inaweza kupunguza gharama ya uagizaji wa mbolea kwa zaidi ya asilimia 50.

Lakini pamoja na matarajio hayo ya serikali na wakulima nchini bado gharama za mbolea sio rafiki kwa wakulima pamoja na bei kushuka mwaka 2019 ukilinganisha na miaka iliopita.

Pamoja na Serikali kusisitiza wakulima kuvitumia Vyama vya Ushirika katika utatuzi wa changamoto za kiuchumi na Kijamii, bado wanaushirika wameshindwa kubuni mfumo madhubuti wa kuwaunganisha katika ununuzi wa Pembejeo ambazo zingewapa unafuu wa gharama za uzalishaji pamoja na kwamba Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, kusisitiza kwamba Ushirika ni chombo pekee cha kumletea mwananchi mnyonge maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Waziri Hasunga amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa Tayari Wizara ya Kilimo kupitia kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania imetoa Waraka wa kuagiza Vyama vyote vya Ushirika kupeleka mahitaji yao ya mbolea kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili iagizwe kwa pamoja kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS – Bulk Procurement System).

Endapo Vyama vya Ushirika vitaagiza mbolea kupitia BPS kwa kutumia dhamana za Benki (Bank guarantees) zenye tozo ndogo (asilimia 1 – 4) na kusafirisha mbolea kwa pamoja kwa njia ya reli, gharama zitapungua na mbolea ya NPK itakuwa na bei ndogo kuliko DAP.

Amesema Vyama vya ushirika vinapaswa kuwa ndio kimbilio la wakulima na hivyo kuagiza mbolea kwa pamoja itapelekea kupungua kwa gharama za mbolea na ziweze kufika kwa wakati.

Kadhalika, katika mkutano huo Waziri Hasunga ameiagiza Taasisi ya Utafiti na udhibiti wa Viuatilifu katika ukanda wa kitropiki TPRI kutoa mafunzo kwa wananchi nchini kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe John Palingo akimuwakilisha mkuu wa mkoa wa Songwe katika mkutano huo ameipongeza serikali kwa kuanzisha na kuvisimamia vyama vya ushirika nchini kwani kupitia umoja huo wakulima wameendelea kunufaika ikiwa ni pamoja na kuwa na bei nzuri ya mazao.

Amesema kuwa pamoja na mambo mengine lakini pia ushirikuwa mkombozi kwa wakulima kwani unawasaidiia wakulima kupata tija ya mazao na kuimarisha kipato chao.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527