TAMASHA LA SAUTI ZA BUSARA LIMEWADIA ZANZIBAR


Na Andrew Chale - Dar
TAMASHA la Sauti za Busara linaloanza Februari 13 hadi Februari 16, mwaka huu limekuja na kauli mbiu kupinga ukatili wa kijinsia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmud alisema kuna kila sababu ya kusherehekea, ikizingatiwa kuna mkusanyiko wa tamaduni mbalimbali za muziki wa Afrika na fursa zinazoendelea kupatikana kutoka kwenye tamasha hilo. 

Tamasha la mwaka huu linaunga mkono juhudi za kukuza muziki unaopigwa mubashara wakati huo huo kukemea unyanyasaji wa kijinsia, suala ambalo linaendelea kutesa tasnia ya muziki na jamii kwa jumla.

"Suala hili la unyanyasaji wa kijinsia litashughulikiwa chini ya kauli mbiu isemayo 'Paza sauti yako, sema hapana kwa unyanyasaji wa kijinsia".

"Kampeni ya 'Paza Sauti' inakusudia kubadilisha mitizamo, kuhamasisha mazungumzo, na kuhimiza heshima kwa wanawake kwa kukuza uelewa juu ya udhalilishaji wa kijinsia.

"Hivi sasa nchini Tanzania, tunaona ni wanawake wachache tu wanaofanya muziki wa asili na wenye kuvutia. Hii ndiyo sababu kwa tamasha la Sauti za Busara la 2020 tulichagua wasanii kama Siti & the Band (Zanzibar) 

Thaïs Diarra na Mamy Kanouté (kutoka Afrika Magharibi), Pigment (Reunion), Evon na Apio Moro (Uganda) na wengine kutoka nchi za ukanda wa Afrika Mashariki. 

"Hawa ni wanawake wenye hisia kali ambao hutumia muziki kufikisha ujumbe na kujielezea. Wakati huo huo, bado wote ni waburudishaji wazuri kwa kupiga (live) mubashara, " alisema  Yusuf.

Hata hivyo, alikiri kuwa tamasha moja peke  haiwezi kubadilisha kabisa jamii; 

"Tamasha la Sauti za Busara linaungana na washirika wenye malengo yanayofanana, kukuza mazungumzo, kubadili mitazamo na kuhimiza hatua dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

muziki wa Afrika haujajikita tu katika burudani; unaweza pia kuwa sehemu ya kuwasilisha ujumbe muhimu. 
"Tunatambua jukumu kubwa wasanii wanaloweza kufanya katika jamii, kama wasemaji, wasimulizi, watu wenye maono, wanaharakati na waponyaji. Tamasha hili linaunga mkono uhuru wa kujieleza kwa wanamuziki na hutoa nafasi nzuri ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kufikia hadhira kubwa na nafasi ambazo zinakuza michango yao kwa jamii." Alimalizia Yusuf.

Kwa upande wake,  Meneja wa tamasha hilo, Journey Ramadhan alisema kwa karibu miongo miwili Tamasha la Sauti za Busara limekuwa mstari wa mbele katika kuitangaza Zanzibar na Tanzania duniani, kuvutia watangazaji wa kimataifa na kutoa fursa kwa wanamuziki kuonyesha kazi zao kwa hadhira ya kimataifa.

"Tangu mwaka 2004 wakati tamasha hili lilipofungua milango yake, lengo letu limekuwa kuonyesha muziki ambao ni wa kipekee na wenye utambulisho wa utamaduni. Tumefanikiwa kuonyesha mfululizo kuwa kuna soko na mahitaji ya sauti mpya zinazovutia za asili ambazo ni za kipekee, "alisema.

Na kuongeza kuwa, Orodha ya wanamuziki watakaotumbuiza mwaka huu inabeba ladha za muziki wa aina zote na watumbuizaji wengi watakuwa wakitumbuiza kwenye tamasha hilo la Sauti za Busara kwa mara ya kwanza. 

Wasanii hao ni pamoja na:
 Mehdi Qamoum (Morocco), OumarKonaté (Mali), Blinky Bill (Kenya), Guiss GuissBou Bess (Senegal), The Mafik (Tanzania), Ambasa Mandela & The Last Tribe (Kenya).

Pia wapo Wakazi (Tanzania), Mamy Kanouté (Senegal), Onipa (Ghana/Uingereza), Thaïs Diarra (Senegal / Uswisi), Mradi wa Mehdi LaifaouiTrab (Algeria), Sibusiso 'Mash' Mashiloane (Afrika Kusini), Nadi IkhwanSafaa (Zanzibar), Siti & the Band (Zanzibar), SeunOlota (Nigeria), Pigment (Reunion), Mannyok (Morisi), FRA! (Ghana), TaraJazra (Zanzibar), Apio Moro (Uganda), IsonMistari aka Zenji Boy (Zanzibar).

Kaloubadya (Reunion), Lulu Abdalla (Kenya), Mapanya Band (Zanzibar), SinaUbi & Zawose Ghost Group (Tanzania), Evon (Uganda) ), RahatZamaan Taarab Orchestra (Zanzibar), Mopao Swahili Jazz (Tanzania) na wengine zaidi.

Tamasha la 17 la Sauti za Busara, kwa mwaka huu linadhaminiwa na Ubalozi wa Norway, Africalia, Ubalozi wa Falme za Uholanzi, British Council, Shirika la Vyombo vya Habari la Zanzibar, Zanlink, Memories of Zanzibar, Ubalozi wa Ufaransa, Emerson Zanzibar, Redio ya Chuchu FM, Mozeti, Music In Africa na wengine zaidi.

Tiketi na taarifa zinapatikana kupitia: www.busaramusic.org

Tamasha hilo jukwaa kuu litakuwa katika eneo la kihistoria la Ngome Kongwe (Old Fort), ambapo watazamaji wataweza kupata burudani ya aina yake ya muziki mubashara kutoka katika majukwaa matatu tofauti.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527