STAMICO KUANZISHA MRADI WA KUSAFISHA DHAHABU MWANZA


Imeelezwa kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lipo katika hatua za awali za uanzishwaji wa Mradi wa Kusafisha Dhahabu (Gold Refinery) na tayari kampuni ya ubia ijulikanayo kama Mwanza Precious Metals Refinery Company Limited imeanzishwa.


Hayo  yamebainishwa  Januari 21, 2020 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa (STAMICO) Dkt. Venance  Mwase wakati  akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya shirika hilo kwa  Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa niaba ya Waziri wa Madini.

Dkt. Venance ameileza kamati hiyo kuwa,  mradi huo utaendeshwa kwa ubia ambapo STAMICO itakuwa  na hisa asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75, huku ikilelezwa kwamba, mradi huo  utakaojengwa jijini Mwanza utahusisha kujenga mtambo wenye uwezo wa kusafisha wastani wa kilo 200 hadi 500 kwa siku.

Ameongeza kuwa, makadirio ya fedha zinazohitajika ni Dola la Marekani Milioni 58.204 ambazo zimepangwa kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kusafishia dhahabu, gharama za awali za mradi, kununua dhahabu kutoka katika masoko pamoja na gharama zaza uendeshaji na kuongeza‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti tumepanga uwe mtambo wa viwango vya kimataifa,’’.

Aidha, Dkt. Mwase amesema kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019, tayari mradi umetekeleza majukumu kadhaa ikiwemo kupata leseni ya kujenga na kuendesha mtambo huo, kusainiwa mkataba wa ubia pamoja na kuanza taratibu za uanzishwaji wa kampuni ya ubia na kupata eneo la ujenzi wa mtambo chini EPZA. 

Ameongeza majukumu mengine yaliyotekelezwa ni pamoja na kufanyika kwa Athari kwa Mazingira (EIA) kwenye eneo la mradi upembuzi yakinifu pamoja na kukusanya taarifa za upatikanaji wa dhahabu katika maeneo mbalimbali yanayokusudiwa.

Akizungumzia shughuli nyingine zinazoendeshwa na Shirika hilo amesema linaendelea kutoa huduma za Kibiashara za uchorongaji miamba wa biashara katika sekta ya mafuta na gesi ambapo katika Mwaka wa Fedha 2019/20  ambapo limefanikiwa kupata kandarasi 4 za uchorongaji kupitia zabuni mbalimbali  zenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 .

Kuhusu Mgodi wa Stamigold ambao ni Kampuni Tanzu ya Shirika hilo ameieleza kamati hiyo kuwa, kuanzia Julai hadi |Desemba, 2019, mgodi huo umezalisha na kuuza wakia 7,133.00 za madini ya dhahabu na wakia 879.19 za madini ya fedha, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 24,172,700,255.34.

‘’ Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hicho, mgodi umelipa jumla ya shilingi 1,712,455, 550.91 kwa ajili ya malipo ya mrabaha, ada ya ukaguzi na kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi,’’ ameeleza Dkt.  Venance.

Kuhusu mradi wa makaa ya mawe katika Mradi wa Kabulo na Kiwira, amesema jumla ya tani 4,359.10 ziliuzwa na kulipatia Shirika kiasi cha shilingi 17,558,184.76 na kuongeza kuwa, ‘’ shirika lilifanikiwa kulipa mrabaha, ada ya ukaguzi na tozo ya Halmashauri ya jumla ya shilingi 23,645,000.62

Aidha ameongeza kuwa Mgodi umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 400.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na kamati, amewatoa Hofu Wajumbe wa kamati hiyo kuhusu Maendeleo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo ameeleza pamoja na changamoto zinazolikabili, linakua na linafanya vizuri.

Waziri Biteko ameiomba Kamati hiyo kuendelea kuilea na kuishauri STAMICO  kwa kuwa mwelekeo wake ni mzuri na kwamba hivi sasa lina uwezo wa kuzalisha hadi shilingi Bilioni 20 tofauti na ilivyokuwa awali na kuongeza kuwa, Watendaji na Bodi ya Shirika hilo mara zote wanafanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati pamoja na Wizara.

‘’Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa bahati mbaya sana kulifuta shirika hili. Linakua, wanaendelea vizuri na Wana Bodi nzuri, watendaji wanasikiliza ushauri na kuufanyia kazi na mapungufu yanafanyiwa kazi, naomba muendelee kuilea na kuishauri STAMICO,’’amesisitiza Waziri Biteko.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527