SERIKALI KUTOINGILIA TAALUMA YA UKAGUZI WA HESABU ZA FEDHA

Na. Josephine Majura na Peter Haule WFM, Dodoma

Serikali imeeleza kuwa haina mpango wa kuingilia taaluma ya ukaguzi wa hesabu nchini kwa kuondoa kipengele cha Hati inayoridhisha kwenye Ukaguzi wa Hesabu kwa kuwa ni matakwa ya Viwango vya kimataifa vya uandaaji wa Taarifa za Fedha.

Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bunda Mhe. Mwita Boniface, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaondoa kipengele cha Hati safi kwenye taarifa za ukaguzi wa Hesabu za Fedha kwa kuwa ni dalili za kuficha ubadhirifu katika Mashirika na Taasisi za Umma.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Kijaji, alisema kuwa kutoa utaratibu mwingine wa taarifa za kikaguzi za fedha itakua ni kukiuka Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Fedha (IPSAS) katika Sekta ya Umma na pia Viwango vya Kimataifa vya Ukaguzi (ISSAI) ambavyo Serikali imeviridhia.

“Dhana ya kuwa Hati inayoridhisha inatoa tafsiri ya kuwepo kwa kila aina ya ubadhirifu siyo sahihi kwa sababu maoni ya ukaguzi yanatolewa kwa malengo maalum ya kuwafahamisha watumiaji wa taarifa za fedha kama taarifa hizo zinaonyesha ukweli na hali halisi ya hesabu za mizania kwa taarifa za mapato na matumizi pamoja na taarifa ya mtiririko wa fedha kwa kipindi kilichokaguliwa”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa Hati inayoridhisha hutolewa kwa Taarifa za Fedha zinazowasilishwa na kukaguliwa zinapozingatia Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Sekta ya Umma na Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa dhana ya ukaguzi wa Hesabu inajikita katika masuala ambayo wakaguzi wanaamini kuwa ni mazito na yanaathari kubwa kwenye taarifa za fedha za Taasisi husika.

“ Lengo Kuu la ukaguzi wa Hesabu ni kutoa maoni kama Hesabu zinazokaguliwa zinaonesha hali halisi ya mapato na matumizi ya Serikali kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uandaaji wa taarifa za fedha”, alifafanua Dkt. Kijaji.

Alifafanua kuwa Maoni hutolewa kwa njia ya hati za ukaguzi ambazo zimegawanyika katika makundi manne ambayo ni Hati inayoridhisha, Hati yenye shaka, Hati isiyoridhisha na Hati Mbaya.

Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 inampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya kaguzi mbalimbali ambazo ni Ukaguzi wa Hesabu (Financial Audits, Ukaguzi wa Kiuchunguzi (Forensic Audits), Ukaguzi wa Ufanisi (Performance Audtis) na Ukaguzi Maalum (Special Audits) ili kujua hali halisi ya Mapato na Matumizi.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post