NAIBU WAZIRI MABULA AAGIZA WAKUU WA IDARA HALMASHAURI ZA MKOA WA NJOMBE KUANDIKIWA BARUA ZA KUJIELEZA

Na Munir Shemweta, WANMM NJOMBE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza Wakuu wote wa idara za Ardhi katika Halmashauri za mkoa wa Njombe kuandikiwa barua za kujieleza kutokana na kushindwa kusimamia uingizaji taarifa za viwanja kwenye mfumo wa Kielektroniki wa ukusanyaji kodi ya serikali.

Aidha, alitoa miezi mitatu kuanzia tarehe 11 Januari 2020 hadi April 12, mwaka huu kwa halmashauri za mkoa wa Njombe kumpatia taarifa ya kuingizwa viwanja vyote vya wamiliki wa ardhi kwenye mfumo wa kielektroniki katika mkoa huo.

Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana katika kikao chake na watendaji wa sekta ya ardhi wa halmashauri sita za mkoa wa Njombe akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Wakuu wa idara ya ardhi walioangukia mikono ya Dkt Mabula kuhusiana na kuandika barua za kujieleza ni kutoka Halmashauri za Njombe Mji iliyoingiza viwanja 7,301, Makambako 5,712, Njombe Wilaya 326, Wanging’ombe 375, Makete 2156 na Ludewa viwanja 3,793.

Uamuzi wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi unafuatia kuelezwa kupitia taarifa ya mkoa wa Njombe pamoja na zile za halmashauri zote za mkoa huo kuwa, kuanzia kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 ni  viwanja 19,645 tu ndivyo vilivyoingizwa kwenye mfumo kati ya viwanja 40,961.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki ulianza mwaka 2017 lakini cha kushangaza hadi kufikia sasa hakuna jitihada za dhati zilizofanywa na baadhi ya halmashauri kuhakikisha viwanja vyote vinaingizwa kwenye mfumo huo ili kurahisisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia pango la ardhi.

Alisema, kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki siyo tu unarahisisha kutambua wamiliki wote wa ardhi bali unasaidia kuwafuatilia wamiliki wanaokwepa kilipa kodi ya ardhi jambo alilolieleza lisiposimamiwa kwa umakini litapunguza wigo wa ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

‘’Uingizaji viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki ulianza tangu mwaka 2017 lakini bado hakuna kilichofanyika hatuwezi kulea uozo huu unaoweza kuwapa mzigo wateja kutokana na malimbikizo ya kodi’’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri Mabula alisema, wizara yake inataka kuwa na malengo yanayoendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano na kuiagiza ofisi ya Ardhi ya Kanda kupitia takwimu za viwanja vilivyo katika mfumo kwa halmashauri za mkoa wa Mbeya na kusisitiza haiwezekani kuwa na Afisa Ardhi Mteule ama Mkuu wa idara ya Ardhi asiyefuatilia na kusisitiza katika suala hilo wizara yake haitakuwa na msamaha.

Akigeukia ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula alionesha kutoridhishwa na makusanyo ya kodi hiyo kwa halmashauri za mkoa wa Njombe ambapo kufikia Desema 2019 halmashauri zote zilikusanya jumla ya shilingi 369,863,643.34 kiasi alichokieleza kiko chini ya asilimia 50 ya makusanyo ya kodi ya ardhi katika mkoa huo uliokuwa na lengo la Bilioni 1.2.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa gharama ya takriban bilioni 2.7.

Dkt Mabula mbali na kuridhishwa na ujenzi wa jengo hilo amelitaka shirika la Nyumba la Taifa kuhakikisha jengo hilo linakamilika mapema iwezekanavyo kwa kuwa lilichelewa kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post