BABA AUA MTOTO WA MIAKA MITATU KWA KUMCHARANGA MAPANGA BUKOBA

Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Ashura Jumapili - Malunde 1 blog Bukoba
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Leonard Kishenya anatuhumiwa kumuua kikatili mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka mitatu kwa kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kutenganisha mkono wa kushoto.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 03,2020 ofisini kwake  Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera (ACP )Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea Januari mosi mwaka huu ,usiku wa kuamkia mwaka mpya saa 6:40 usiku katika kijiji cha Katorerwa Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera ambapo mtoto Careen Crispine mwenye umri wa miaka (03) aliuawa.

Alisema marehemu alikuwa anaishi na mama yake mzazi aitwaye Domina Andrew (30 )aliyekuwa ameolewa na Leonard Kishenya (36 ) ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya mtoto huyo.

Alisema kabla ya tukio hilo la mauaji wanandoa hao walitoka kwenda kwenye mkesha wa mwaka mpya wa 2020 walikuwa wanakunywa pombe na walirudi nyumbani majira yasaa 6:40 usiku na walipofika kulitokea ugomvi kati ya wanandoa hao ambao chanzo chake hakijafahamika.

Kamanda Malimi alieleza kuwa kutokana na ugomvi huo kuwa mkali, mke aliamua kukimbia na kwenda kulala kwa jirani na kumuacha mtoto wake ndani akiwa amelala.

Alisema Januari Mosi mwaka huu majira ya saa moja asubuhi mke alirudi nyumbani na kushuhudia mtoto wake akiwa ameuawa kwa kukatwakatwa na kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake kama vile kichwani na kuutenganisha mkono wa kushoto na mwili.

"Mwili wa mtoto huyo ulikutwa umelala kifudifudi nje ya nyumba yao wakati alikuwa, amelala ndani. Mume ambaye ni mtuhumiwa wa tukio hilo hakuwepo na alikuwa ametorokea kusikofahamika",alieleza.

Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kumkamata na wanaendelea kumhoji chanzo cha kufanya mauaji ya kikatili kwa mtoto asiyekuwa na hatia naatafikishwa mahakamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527