PAUL MAKONDA APIGWA MARUFUKU KUINGIA MAREKANI

Paul Makonda

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, apigwa marufuku kuingia Marekani.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani leo Ijumaa, Januari 31 2020 marufuku hiyo pia inamhusisha mke wa Makonda Bi Mary Felix Massenge.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makonda anashutumiwa kwa kushiriki katika ukandamizaji wa haki za binadamu.

Ukandamizaji wa haki ambao Makonda anashutumiwa kuutenda ni pamoja na kunyima watu haki ya kuishi, haki ya uhuru wa kujiamulia mambo na usalama wa watu.

"Wizara ina taarifa za uhakika kuwa Makonda amehusika katika uvunjifu huo wa haki kupitia nafasi yake kama mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam. Katika nafasi yake hiyo, pia amelaumiwa kwa kukandamiza upinzani wa kisiasa, kukandamiza haki ya kujieleza, na kushambulia makundi yasiyo na sauti," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Michael Pompeo ametumia mtandao wake wa Twitter kutangaza marufuku hiyo.
"Leo tumetangaza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Christian Makonda kuwa hataruhusiwa kuingia Marekani kwa kushiriki kwake katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Tuna wasiwasi mkubwa juu ya kuporomoka kwa heshima ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania," ameeleza Pompeo katika ujumbe wake huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post