KAMATI YA PIC YAITAKA BENKI YA NMB KUANGALIA UWEZEKANO WA KUONGEZA GAWIO KWA SERIKALI

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Kamati ya  kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa mitaji ya umma [PIC] imeitaka benki ya NMB kuangalia uwezekano wa kuongeza gawio kwa serikali hali itakayosaidia  kuongeza mapato katika kuchangia mfuko mkuu wa Serikali.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa mitaji ya umma [PIC] Dkt Raphael Chengeni amesema hatua hiyo itafanikisha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo hapa nchini.

Katika hatua nyingine Dkt Chengeni amemuagiza mwenyekiti wa bodi ya benki  ya NMB  Profesa Joseph Semboja kuhakikisha anapeleka mbele ya kamati hiyo mchakato mzima  wa kumpata mtendaji mkuu wa benki hiyo ili kutoa fursa kwa watanzania wenye uwezo na weledi wa kuongoza taasisi kubwa za kifedha wanajitokeza kwa ajili  ya maslahi mapana ya taifa .

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth Zaipuna amesema benki yake inaunga mkono miradi mikubwa ya kimkakati ya serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ili kurahisisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja  .

Kamati  mbalimbali za bunge zinaendelea na vikao vyake jijini dodoma tangu Januari 13,2020 huku kikao cha 18 cha Bunge  kikitarajia kuanza Januari ,28,2020.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post