IRAN YAKIRI KUIDUNGUA KWA KOMBORA NDEGE YA UKRAINE


Iran imekubali kuwa iliidungua kwa kombora Ndege ya Ukraine iliyoua Watu 176  siku ya Jumatano, runinga ya taifa ya Iran imeripoti.

Taarifa ya jeshi inaeleza kuwa mkasa huo umetokana na "makosa ya kibinadamu" baada  ya ndege hiyo kupita karibu na eneo nyeti linalomilikiwa na Kikosi cha Mapinduzi (Revolutionary Guards). Maafisa waliofanya kosa hilo wataadhibiwa, taarifa hiyo imeeleza.

Iran awali ilikanusha vikali taarifa kuwa moja ya makombora yake yaliitungua ndege hiyo karibu na mji mkuu Tehran. Watu wote 176 ndani ya ndege hiyo wamepoteza maisha.

Hata hivyo nchi hiyo ilibanwa zaidi  baada ya Marekani na Canada kudai kuwa taarifa za kijasusi walizonazo zinaonesha kuwa Iran iliidondosha ndege hiyo kwa bahati mbaya na moja ya makombora yake.

Kuanguka kwa ndege hiyo kulitokea saa chache baada ya Iran kushambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq kwa makombora ya masafa marefu.

Vyombo vya habari vya Marekani vinadai kuwa Iran ilidhani kuwa ndege hiyo ilikuwa ya kivita ya Marekani, wakati taifa hilo lilipokuwa ikijiandaa kujibu mashambulio dhidi ya Marekani baada ya wao kushambulia vituo vyake vya kijeshi nchini Iraq kwa makombora.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527