DKT NCHIMBI ATEMA CHECHE

-
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi, akiwahutubia watumishi wa Umma wa mkoa wa Singida leo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, akiangalia jinsi mkorosho wa miaka 2 ulivyotoa korosho katika shamba  la pamoja (block farming) wilayani Manyoni alivyotembelea Mkoa wa Singida hivi karibuni. Mhe. Majaliwa alipongeza ubunifu huu uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Singida ambapo  hadi sasa takribani hekta 12000 zimepandwa mikorosho na hakuna mkoa wowote hapa nchini ambao umebuni  mfumo huu kwenye zao lolote.
Na John MapepeleMkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi amesema kuwa  kila mtumishi  wa Serikali  katika mkoa wake kuanzia mwaka huu 2020 atatakiwa kuonyesha mafanikio yanayotokana na  mishahara wanayolipwa na Serikali kupitia kauli mbiu maalum  iliyoandaliwa na mkoa ya “mshahara wangu upo wapi” ifikapo mwisho wa mwaka  huu.

Pia aliwaonya kuachana na mambo ya siasa na badala yake kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa  Rais John Pombe Magufuli.


Akizungumza na watumishi wa Umma  wa mkoa wa Singida katika mkutano maalum wa kwanza katika mwaka  huu 2020 mjini Singida leo ambapo Dk. Nchimbi alisema mkoa huo umeamua kuiishi kauli mbiu hii baada ya kuona mafanikio ya kupigiwa mfano yaliyopatikana kutoka kwa wanufaika wa mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)  ulilenga  katika kunusuru kaya masikini na baada ya muda wa mradi  waweze  kusimama wenyewe uliozinduliwa Septemba, 2014  mkoani hapo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa.


Alisema katika  mpango huo ruzuku ya shilingi elfu ishirini(20,000/=) ilitolewa kwenye kila Kaya yenye sifa katika Halmashauri 6 kati ya 7 za mkoa pamoja na fedha za masharti ya afya na elimu ambayo  kila kaya yenye mtoto anayesoma Shule ya Msingi  na Sekondari na wale  chini ya miaka 5 walipewa  kuanzia shilingi elfu mbili(2000) hadi elfu sita (6000), ambapo alisema ruzuku hiyo imekuwa  msaada mkubwa kwa kaya masikini katika kuwanunulia  sare, madaftari pamoja na kulipia matibabu hasa  kujiunga Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii(NHIF).Aliongeza kuwa hadi kufikia mwezi Januari 2020, jumla  ya kaya 38,136 kutoka katika vijiji 278 zinanufaika na ruzuku hii na jumla ya shilingi  takribani bilioni thelathini na saba na milioni mia tisa (37,900,000,000) ziliwafikia walengwa.


“Napenda kuwahakikishia kuwa  hakuna kipindi ambacho watumishi wa umma watakuwa na  maisha bora kama hiki kwa kuwa Serikali ya awamu ya Tano imeshaboresha kwenye kila sekta kama miundombinu,huduma za afya, elimu itashindwaje kuboresha maisha ya watumishi umma” alihoji Dk. Nchimbi huku akisisitiza kuwa watumishi wazembe hawatavuka mwaka 2020 wataondolewa mara moja kupisha watumishi wanaoendana na kauli mbiu ya hapa kazi  tu.


Aidha Dk. Nchimbi alisema pamoja na kuhakikisha kuwa mishashara ya watumishi inaleta tija kwenye familia na kuboresha uchumi, tayari mkoa unatekeleza  mikakati mahususi ya  kilimo cha kisasa  cha pamoja cha zao la korosho kwa wananchi  wa Mkoa wa Singida  ambapo ametoa rai kwa watumishi na wananchi kujitokeza ili kupatiwa maeneo hayo ili kuyaendeleza kwa pamoja.


“Hadi sasa Singida siyo, masikini, kame wala yenye njaa kama iliyokuwa ikitafsiriwa na baadhi ya watu hapo awali. Tayari hekta elfu kumi na mbili (12000)  za kilimo cha pamoja (block farming) zimepandwa mikorosho na zimeanza kuzaa korosho katika Wilaya ya Manyoni. 

Ninatoa shukrani na  pongezi zangu za dhati kwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutupatia pikipiki 10 ili ziweze kusaidia katika kazi hii” alisisitiza Dk.Nchimbi


Alisema kutokana na tafiti zilizofanyika hivi karibuni zimeonyesha kuwa ardhi ya mkoa wa Singida ina ubora mkubwa wa kusitawisha zao la Korosho kwa muda mfupi ukilinganisha na maeneo mengi hapa nchini hivyo hakuna sababu ya watumishi na  wananchi kutochangamkia fursa hiyo adimu ambapo pia alionya kuwa wananchi ambao watabainika kuwa hawapo makini wataondolewa katika program hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post