WATU 37 WALAZWA BAADA YA KULA CHAKULA CHENYE SUMU MSIBANI DODOMA


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi akimjulia hali mmoja wa wagonjwa waliolazwa Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa kile kinachodaiwa kula chakula chenye sumu.
Mkuu wa Wilaya Dodoma (kushoto) Mhe Patrobas Katambi akiwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Devis Mwamfupe baada ya kufika hospitalini hapo kujionea hali za wagonjwa 37 waliofikishwa na kulazwa baada ya kudaiwa kula chakula chenye sumu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi (mwenye koti la suti) akiwa na wauguzi na madaktari wa Hospitali ya Rufaa Dodoma alipofika kuwajulia hali wagonjwa waliofikishwa hospitalini hapo ambao wamepata mgonjwa wa kuhara na kutapika wakihisiwa kula chakula chenye sumu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Best Magoma akizungumza na wandishi habari juu ya tukio la kulazwa kwa watu 37 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kile kinachoelezwa kula chakula chenye sumu.
Watu mbalimbali walioleta wagonjwa wao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakisubiri kupata huduma kwenye kitengo cha dharura.
***
Charles James, Michuzi TV

Watu 37 wamefikishwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General Hospital) kwa ugonjwa wa kuhara na kutapika baada ya kula chakula kinachosadikiwa kuwa na sumu.

Tukio hilo limetokea jioni ya leo katika eneo la Mtumba nje kidogo ya Manispaa ya Jiji la Dodoma ambapo walikula chakula hicho wakiwa kwenye msiba wa jirani yao.

Akizungumza hospitalini hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi amekiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza tayari ameshaagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi kwenye mabaki ya chakula hicho ili kugundua chanzo chake.

"Mara baada ya kupata taarifa hizi tumefika hapa na Timu ya viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa kwa hatua ya awali tumesimamia kuhakikisha watu wetu wanapata huduma ya kwanza na kiukweli wagonjwa wote wanaendelea vizuri.

Kati ya hao 37 waliolazwa, wanaume ni 10, wanawake wapo 23 na watoto wakiwa ni wanne, tayari nishatoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo, lakini pia tunafanya uchunguzi wa kitabibu kujua ni sumu ya mtu kuweka au ni sumu ya chakula," Amesema Mhe Katambi.

Amewataka wananchi kuwa watulivu kwa sasa na kusubiria kupata majibu kutoka kwa Timu inayofanya uchunguzi na kuwataka wale wote ambao wanaona dalili za kuhara na kutapika kufika katika vituo vya afya vilivyopo karibu ili kupatiwa matibabu.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Best Magoma amesema hali ya wagonjwa waliofikishwa hospitalini hapo inazidi kuimarika baada ya kuwapatia matibabu na pindi watakaporidhishwa na maendeleo ya afya zao wataruhusiwa kurudi majumbani mwao.

" Tunawashukuru viongozi wetu wa ngazi ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya kwa kufika hapa na kutuongezea nguvu, na timu yetu kwa kushirikiana na wenzetu wa Polisi na TBS tumeshaanza uchunguzi wa kubaini nini chanzo cha tatizo hili, nitoe wito kwa wananchi ambao wanaona dalili kama hizi kujitokeza haraka kwenye vituo vya afya na sisi tupo tayari kuwahudumia," Amesema Dk Magoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post