WANAUME SHINYANGA WAKIRI KUUZA MAZAO KUFANYA NGONO NA WANAWAKE WEUPE


Peter Shilinde maarufu 'Ndizi/Banana' akitoa ushuhuda jinsi alivyokuwa anauza mazao nyumbani na kwenda kununua wanawake weupe.
Chapa Mamba akitoa ushuhuda jinsi alivyokuwa anauza mazao nyumbani na kwenda kununua wanawake.

Na Marco Maduhu - Shinyanga

Baadhi ya wanaume wa kijiji cha Butini Kata ya Itwangi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamekiri kuuza mazao ili kununua ngono kutoka kwa wanawake (Makahaba), ambao hutoka mijini kwenye kipindi cha mavuno na kwenda vijijini kwa ajili ya kufanya biashara ya ngono ili kuchuma fedha za mavuno kutoka kwa wanaume wa kijiji hicho.

Wamedai kuwa kinapofika kipindi cha mavuno ya mazao hua kuna ongezeko la wanawake wengi weupe kutoka mjini, ambao hufika kijijini humo kwa ajili ya kufanya biashara ya kuuza ngono, ambapo baadhi yao hushawishika na kuamua kuuza mazao na kumpatia fedha mwanamke ambaye amempenda na kushiriki naye ngono.

Mmoja wa wanaume kijijini hapo Peter Shilinde maarufu 'Ndizi/Banana' ambaye ana watoto wanne, ametoa ushuhuda kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
yaliyofanyika Desemba 11,2019 yaliyoandaliwa na Shirika la Kivulini ambalo linatetea haki za wanawake, kuwa yeye ni miongoni mwa wanaume ambao walikuwa wakinunua makahaba kutoka mjini lakini sasa ameachana na tabia hiyo.

Amesema kutokana na makahaba hao kuhitaji fedha nyingi ili wafanye nao mapenzi, kuanzia shilingi 80,000 hadi 100,000, iliwalazimu kuuza mazao yao ya mpunga na kuwapatia fedha hizo ambazo wanazihitaji na kisha kushiriki nao ngono na kama mwanaume hana fedha itabidi ampatie gunia zima la mpunga.

“Kuna tatizo kubwa hapa kijijini kwetu la wanaume kuuza mazao na kwenda kununua ngono kwa makahaba ambao huja vijijini kufanya biashara hiyo kwenye kipindi cha msimu wa mavuno, na mimi nilikuwa ni miongoni mwao lakini nimeshaacha baada ya kuona nazidi kuwa maskini tu,” amesema Shilinde.

“Na wanaume ambao hua wananunua mahakahaba ni wale ambao wanaendekeza masuala ya ulevi, na ukiuza tu mazao unaikimbia familia na kuhamia Sentani kwa muda wa siku mbili au tatu kwenye maeneo ambayo wanaishi makahaba hao, fedha zikiisha unarudi nyumbani kuuza tena mazao mengine”alisema.

Naye Chapa Mamba alisema kutokana na elimu aliyoipata kupitia shirika la Kivulini alishaacha kuuza mazao nyumbani na kubainisha kuwa vitendo hivyo vinachangia ukatili wa kijinsia.

Teleza Kazilo ambaye ni mhanga wa matukio hayo, amesema mume wake alikuwa na tabia hiyo ya kuuza mazao na kwenda kununua ngono kwa mahakaba wa mjini, na alipokuwa akipinga kitendo hicho alikuwa akiambulia kipigo hadi chakula kinaisha ndani, na kuamua kwenda kufanya vibarua ili watoto wapate chakula.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Masanja Ikingo na Mtendaji wa Kata ya Itwangi Claudia Kimaro, kwa nyakati tofauti wamekiri kuwepo na vitendo hivyo na kubainisha lakini wameshindwa namna ya kuwadhibiti makahaba hao ikiwa hua wanakwenda na njia ya kufanya biashara ya kuuza Pombe ama kununua mpunga.

Aidha Ofisa Tathimini na ufuatiliaji kutoka Shirika la Kivulini, Godfley Paschal, amesema kijiji hicho cha Butini ni miongoni mwa vijiji vilivyopo kwenye Kata ya Itwangi, ambavyo vinapewa elimu ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia, ikiwamo hali ya kiuchumi kwa wanaume kuuza mazao yote na kununua ngono.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527