WAFUNGWA 96 MKOANI SONGWE WAPATA MSAMAHA WA RAIS


Wafungwa 96 Mkoani Songwe wamekuwa miongoni mwa wafungwa Zaidi ya 5000 waliopatiwa msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kufuatia maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika jana jijini Mwanza.

Mapema leo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amefika katika gereza la Mbozi ambapo wafungwa 45 wanapatiwa msamaha wa Rais huku wafungwa wengine wakiwa katika Magereza ya Wilaya za Ileje na Songwe ambapo amezungumza na wafungwa hao kabla hawapewa ruhusa ya kuondoka gerezani hapo.

“Nimeingia gerezani na kukuta wafungwa waliopata msamaha wa Rais Magufuli wakiwa na furaha na wamempongeza sana Rais wetu, lakini pia wafungwa waliobaki wamefurahia uamuzi wa Rais Magufuli wa kutoa msamaha kwani na wao wana tumaini la kupatiwa msamaha siku za baadae.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.

Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa wafungwa waliobaki wamempa changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na matatizo ya uhaba wa maji na ucheleweshaji wa nakala za hukumu mambo ambayo ameahidi kuyashughulikia haraka iwezekanavyo.

Kamishna Msaidizi wa Magereza Laizack Mfaume Mwaseba amesema amekuwa akipokea malalamiko ya ucheleweshaji wa nakala za hukumu kutoka kwa wafungwa na amekuwa akiwasiliana na mahakimu ili waweze kuzitoa nakala hizo kwakuwa ucheleweshaji huo unawanyima haki wafungwa ya kukata rufaa.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto ya maji katika gereza hilo kuna changamaoto za uhaba wa vitendea kazi na sare kwa wafungwa mambo ambayo tayari wamesha yawasilisha kwa kamishana Mkuu wa Magereza kwa ajili ya utatuzi.

Mmoja wa wafungwa wa gereza la Mbozi Victoria Adam amemshukuru Rais Magufuli kwa msamaha alio mpatia na kumuombea kwa Mungu aendelee kumlinda huku akieleza kuwa amejifunza mambo mengi alipokuwa gerezani na sasa anaenda kuwa raia mwema.

Naye Fred Andrea Daud ambaye amepata msamaha wa Rais Maguufuli amesema bahati aliyoipata ya Msamaha ataitumia vizuri kwa kufanya kazi halali kwakuwa Vijana wengi wamekuwa wakichagua kazi ambazo zinawaingiza katika matatizo

Ameongeza kuwa magereza ni sehemu ya urekebishaji na yeye amerekebika hivyo anawashauri vijana wote wafanye kazi halali ambazo hazitawaletea matataizo kwakuwa kazi halali zipo nyingi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527