RAIS DKT. MAGUFULI APATA TUZO KWA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI WA NCHINI


Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dar es Salaam
Shirika lisilo la Kiserikali la Kuinua Diplomasia ya Uchumi Tanzania (TEDEF) limetambua juhudi na kuthamini kazi anazofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha azma ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025 inafikiwa.  


TEDEF imemtunuku tuzo Rais Dkt. Magufuli  na kuwa miongoni mwa Watanzania 10 waliofanya vizuri kwa kutoa mchango wao katika kuimarisha Diplomasia ya Uchumi wa nchini. 


Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli na kuwakabidhi tuzo hizo watanzania wengine waliomstari wa mbele kuinua diplomasia ya uchumi nchini Desemba 5, 2019 katika ukumbi wa Karimjee uliopo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa Na Michezo Juliana Shonza ameishukuru TEDEF kwa uamuzi wao wa  kushirikiana  na  Serikali  katika kuimarisha diplomasia ya Uchumi nchini. 


 “Diplomasia  ya  Uchumi  ni  Muhimu  kwa  ustawi  wa  Taifa.  Mataifa yote makubwa duniani yameupa umuhimu wa kwanza Diplomasia ya Uchumi ambao umekuwa ni muhimili wa kukuza mataifa hayo. Nanyi TEDEF mmekuwa wazalendo kwa kutambua na kuthamini mchango wa viongozi na wananchi mbalimbali katika kuhakikisha nchi yetu inafikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati” alisema Naibu Waziri Shonza. 


Miongoni mwa kazi zilizomfanya Rais Dkt. Magufuli kupewa tuzo hiyo mchango wake katika kujenga miundombinu ya kufanikisha  Diplomasia ya Uchumi Tanzania ikiwemo miradi ya reli  ya  kisasa (SGR), kuimarisha shirika la  ndege, ujenzi wa barabara na madaraja mbalimbali nchini  pamoja na  Mradi  wa  umeme Bwawa la Nyerere.    


Watanzania wengine waliopata tuzo za kushiriki kujenga diplomasia ya uchumi ni mawaziri wawili ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi kwa kuongoza  majadiliano ya Biashara ya Kimataifa baina  ya Tanzania na Kampuni  ya  Madini  ya Barrick kwa mafanikio makubwa kwa Tanzania pamoja na Wiziri wa Mambo ya Ndani nchi  Kangi Lugora ambaye anasimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kutambua amani iliyojengeka ni muhimu kwa kufanikisha Diplomasia ya Biashara na Diplomasia ya Uchumi.      


Tuzo hizo pia zimeenda kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi ambao nao wametambuliwa kwa mchano wao katika kujenga diplomasia ya uchumi; Ubalozi wa Tanzania Nchini Rwanda ukiongozwa na Balozi Ernest Mangu ambao umeongoza kwa mauzo ya nje katika nchi za Afrika Mashariki, Ubalozi wa Tanzania nchini China ukiongozwa na Balozi Mbelwa Kairuki kwa kwa kuongoza katika uwekezaji mitaji nchini pamoja na Ubalozi wa Tanzania Nchini Marekani ukiongozwa na Balozi Wilson Masilingi ambao umeongoza kwa kuleta watalii nchini. 


Mbali na viongozi hao, Mkoa wa Dar es Salaam ambao unaongozwa na Mkuu wa mkoa huo Paul Makonda nao umepata tuzo hiyo kwa kuongoza kwa miradi  ya uwekezaji ambapo takribani miradi 109 imesajiliwa. 


Aidha, Watanzania wengine ambao wametambuliwa kwa mchango wao katika kushiriki katika kuitangaza Tanzania kimataifa katika diplomasia ya uchumi na kupewa tuzo hiyo ni mchezaji wa mpira wa miguu Mbwana Samata kupitia sekta ya michezo, mwanamuziki Nasibu Abdul (Diamond) kupitia sekta ya muziki pamoja na mtangazaji wa TBC Elisha Elia anayetangaza kipindi cha Kishindo cha Awamu ya Tano  na  kusaidia  kutangaza miundombinu ya Diplomasia ya Biashara na Diplomasia ya Uchumi kupitia sekta ya habari.      

  
Kwa upande wake Mkurugenzi na Makamu Mwenyekiti Bodi ya TADEF Dkt. Wilbroad Mtabuzi ameyataja baadhi ya majukumu ya msingi ya shirika hilo kuwa ni pamoja  na  kuvutia uwekezaji hasa kwenye viwanda, Kuhamasisha biashara ya kimataifa kuhamasisha utalii, kutangaza sifa njema za nchi yetu ambayo  ni amani, utulivu na  umoja wa Kitaifa ambapo majukumu hayo yatasaidia kuchangia kasi yakuufikia uchumi wa kati. 


Dkt. Mutabuzi amesema kuwa TEDEF imefanikiwa kuunda vyama vya ushirika kwa wahimitimu wa elimu ya juu nchini ambao wamejiajiri katika katika sekta ya kilimo-biashara  kwenye  mikoa  ya  mikoa  ya  Dare  es  salaam,  Pwani, Dodoma,  Kigoma,  Mbeya  na  Mwanza.   


Wahitimu hao wamefanikiwa kuanzisha vikundi vya ufugaji samaki kibiashara katika mkoa wa Pwani eneo la Ruvu wilayani Bagamoyo pamoja na kuwasaidia wakulima zaidi ya 2000 wanaojishughulisha na kilimo wamenufaika na huduma za TEDEF nchini. 


Sera ya Diplomasia ya Uchumi Mwaka 2001 nchini ilianza kutekeleza kufuatia idhini ya Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa mwaka 2000 ikitambua kuwa Diplomasia ya Uchumi ni Ustawi ambapo ushiriki wa TEDEF katika diplomasia hiyo una mchango katika kuleta ustawi katika nchini.
-Mwisho-


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527