HUU NDIYO MJI WENYE PAKA WENGI ZAIDI KULIKO WATU


Kundi la paka katika barabara za mji wa Kafr Nabl

Baada ya miezi kadhaa ya mashambulio ya mabomu kutoka kwa vikosi vya Syria na Urusi, mji wa Kafr Nabl nchini Syria sasa umesalia kuwa makaazi ya paka wengi kuliko watu.

Watu wachache waliosalia katika mji huo wa Syria uliolipuliwa wanajiliwaza na mamia au pengine maelfu wa paka, kama ilivyobaini BBC.

Baadhi ya wakaazi hujificha chini ya kifusi cha nyumba zilizobomolewa ili kujikinga dhidi ya mabomu yanayodondoshwa kutoka angani.

Mmoja wao ni Salah Jaar mwenye umri wa miaka 32 (katika picha hapo juu), lakini kama unavyoona hayuko peke yake.

Katika kifusi kilicho karibu naye kuna mamia ya paka waliojipata katoka hali kama yake.

"Unafarijika paka akiwa karibu nawe," alisema. 'Zinafanya sahali milipuko ya mabomu, kuporomoka kwa majengo, mateso, na uwoga."

Nyumbani kwa Salah katika mji wa Kafr Nabl, wakati mmoja ulikuwa makazi ya watu 40,000, lakini sasa ni watu chini ya 100 waliosalia.

Ni vigumu kubaini ni paka wangapi waliopo hapo - ni mamia kwa hakika lakini huenda wamefikia maelfu.Mji wa Kafr Nabl

"Watu wengi sana wamehama mji wa Kafr Nabl hali iliyofanya idadi ya watu kuwa ndogo sana. Kwa kuwa paka wanahitaji watu wakuwatunza kuwapa maji na chakula, wamehamia katika nyumba za watu walioamua kubaki katika mji huo mahame. Kila nyumba ina karibu paka 15, au hata zaidi," Salah anasema.

Salah bado anafanya kazi ya uandishi habari katika kituo cha radio cha, Fresh FM, japo studi za kituo hicho zilibomolewa katika mashambulizi ya angani ya hivi karibuni.

Walikuwa na bahati shughuli za kituo hicho zilihamishiwa mji ulio karibu kutokana na sababu za kiusalama,muda mfupi kabla ya mashambulio hayo.

Kituo hicho ambacho huwatangazia watu kuhusu kitisho cha mashambuliuo kupitia habari, na vipindi vingine kilipata umaarufu kutokana na paka.

Makumi kati ya paka hao walifanya ofisi za kituo hicho kuwa makaazi yao. Muasisi wa kituo hicho na mwanaharakati Raed Fares, aliyeuawa na wanamgambo wa Kiislam wenye silaha mwezi November 2018, alitenga fedha za kuwanunulia maziwa na chakula.

"Paka wengi walizaliwa katika jengo hilo. Mmoja wao aliyekuwa na rangi nyeupe na madoa ya hudhurungi alimpenda sana Raed. Angeliandamana nae kila mahali na hata kulala kando yake," anasema Salah.

Anapondoka katika mabaki ya iliyokuwa nyumba yake, anakaribishwa na sauti za paka kutoka kila upande, Hili humfanyikia kila mtu, anasema.

"Wakati mwingine tunapotembea njiani tunaweza kupatana na paka 20 au 30 wanaoandamana na sisi kila tunapoenda. Baadhi yao walitufuata hadi nyumbani."

Giza linapoingia milio ya mbwa wasio na wenyewe husikika kutoka kila upande wa mji huo. Wao pia wana njaa na hawana pakwenda. Hali ya kupigania mabaki ya chakula na mahali pa kulala inawafanya kushindana na paka wa Kafr Nabl.

Katika makabiliano kati ya paka na mbwa mshindi ni nani?

"Bila shaka mshindi ni paka! Wako wengi sana kuwawaliko mbwa hao." Salah anasisistiza.

Wengi wao walikuwa wanapendwa sana na familia zilizotoroka mji huo baada ya vikosi vya utawala wa Syria kuanzisha oparesheni ya kuukomboa mji wa Idlib mwezi Aprili iliyopita.

Sasa baada ya kukosa wa kuwatunza na chakula cha mara kwa mara wamelazimika kutafuta makaazi mapya chini ya kifusi cha mijengo iliyoporomoka.

Na japo watu kama Salah hawana matumaini ya kuishi, bila kujua chakula kinatoka wapi, wanajiliwaza na paka hawa ambao wamegeuka kuwa marafiki wa dhati.

"Kila ninapokula, nao hula, iwe ni maboga, spageti au hata mkate uliokauka. Katika hali hii nahisi sote ni viumbe wadhaifu na tunahitaji kusaidiana," anasema.

Sio ajabu kwa paka kujeruhiwa pamoja na watu kutokana na mashambulio ya mabomu ya mara kwa mara.

Lakini licha ya uhaba wa dawa, sawa na vifa vingine muhimu, Salah anasema wanajaribu kila wanaloweza kuwatunza paka hao.

"Nina rafiki ambaye anaishi na paka nyumbani kwake. Mmoja wao alijeruhiwa kwa roketi ambayo ilimvunja mguu. Lakini alifanikiwa kumpeleka hadi mji wa Idlib kwa matibabu na sasa anatembea vizuri kama awali,"anasema.

Huku vikosi vya rais Bashar al-Assad vikikaribia Kafr Nabl, mji huo huenda ukavamiwa hivi karibuni. Salah anakiri kuwa na hofu, sio kwake tu bali pia kwa usalama wa paka ambao ni marafiki zake walio wengi.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post