ESTER BULAYA ADAI NDOA YAKE HAIJAVUNJIKA


Mbunge wa Bunda mjini (Chadema) Ester Bulaya ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ndoa yake na muwe wake Gustavu Babile, bado haijavunjika.Ni baada ya kuhojiwa na upande wa mashtaka kama ndoa yake imevunjika au laa.

Bulaya ambaye ni mshtakiwa wa tisa katika kesi ya uchochezi inayowakabili, viongozi waandamizi Chadema, akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ameieleza mahakama hiyo jana Jumatatu Desemba 23, 2019, wakati kesi hiyo lilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa huyo kuhojiwa na jopo la mawakili sita wa upande wa mashtaka


Upande wa Jamhuri uliongozwa na jopo na mawakili wa serikali sita, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, Wakurugenzi wa Mashtaka Wasaidizi, Faraja Nchimbi, Pendo Makondo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Mawakili wa Serikali, Jacqline Nyantori na Salim Msemo.

Akihojiwa na Wankyo, kuhusu maisha yake ya familia, mshtakiwa huyo alidai kuwa alifunga ndoa mwaka 2003 na kwamba kwa sasa anaishi Mbweni na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ni jirani yake.

Akihojiwa na Nchimbi, kuhusu hati yake ya kusafiria alidai, katika hati hiyo hakuna mahali popote palipogongwa muhuri pakionyesha alisafiri nje ya nchi kati ya Februari 16 hadi 28 mwaka 2018.

Alidai alichoieleza mahakama ni kwamba, Februari 16, mwaka jana, aliwahi kuondoka katika mkutano wa kufunga kampeni kwa kuwa Mdee alikuwa anaumwa, hivyo walienda kujiandaa na safari ya kwenda kwenye matibabu Afrika Kusini.

Mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya Buibui, Mwananyamala, Dar es Salaam.

Alidai hajawahi kuieleza mahakama siku waliyosafiri na katika hati yake ya kusafiria imegongwa muhuri katika ukurasa wa 17.

Katika hatua nyingine alidai, hakuna sheria inayoruhusu chama cha siasa kuhamasisha wafuasi wake kudai haki kwa maandamano ama vurugu.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 20 na kusikiliza mfululizo hadi Januari 24, mwakani na shahidi wa 10 wa upande wa utetezi anatarajiwa kutoa ushahidi wake.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Katibu Mkuu wa zamani, Dk. Vicent Mashinji. Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Ester Matiko.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 likiwamo la kula njama, wote wanadaiwa kuwa, Februari 1 na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko la kutawanyika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post