BODI TISA ZA MAZAO KUUNGANISHWA ILI KUUNDA BODI TATU PEKEE


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara
Serikali imedhamiria kuziunganisha Bodi sita za mazao zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo na kuwa na Bodi tatu ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji.


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo jana tarehe 13 Disemba 2019 wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara.

Waziri Hasunga amesema kuwa kumekuwa na Bodi nyingi lakini matokeo ya kiutendaji hayaakisi wingi huo hivyo ili kuboresha majukumu yake na kuwa na weledi katika kazi Bodi hizo zitaunganishwa.

Amesema kuwa Bodi saba zitaunganishwa na kuunda Mamlaka moja ya kusimamia mazao ya kimkakati ambayo ni pamoja na Kahawa, Pamba, Mkonge, Tumbaku, Pareto, Korosho, Alizeti na zao la mchikichi.

Waziri Hasunga amesema kuwa mabadiliko hayo yatakayozihusisha Bodi hizo yatapelekea kuundwa kwa idara za kusimamia kila zao.

Bodi nyingine ya pili itasimamia mazao ya nafaka, mboga mboga na matunda (Cereal and Horticulture Authority) pamoja na Bodi ya Sukari itakayosalia kujitegemea.

Amesema, kuwa na Bodi nyingi kumepelekea usimamizi kuwa mgumu kadhalika kuwa na Bodi chache kutaimarisha ufanisi na uwezo wa kuwasimamia watendaji wake.

Sambamba na hayo Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika mchakato wa kupitia upya sheria ya Ushirika pamoja na Shirika la ukaguzi wa vyama vya Ushirika-COASCO ili kuimarisha sheria na kuwa na usimamizi madhubuti wa mali za wananchi kwenye Ushirika.

Waziri Hasunga yupo mkoani Mtwara kwa ajili ya ziara ya kikazi ambapo awali alitembelea mkoa wa Pwani na Lindi kwa ajili ya kukagua hali ya uuzaji wa korosho msimu wa 2019/2020, kukagua hatua zilizofikiwa za malipo ya wakulima wa korosho zilizonunuliwa na serikali msimu wa mwaka 2018/2019 na kukagua skimu za umwagiliaji.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527