BODI AMBAZO HAZITAWASILISHA GAWIO IFIKAPO JANUARI 23 ZITAKUWA ZIMEVUNJWA

 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipokea hundi ya kiasi cha Sh. Milioni 200, kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Bw. Patrick Ngwediagi, katikati ni Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, wakati wa halfa ya kupokea gawio jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma wakati wa hafla ya kupokea gawio la kiasi cha sh. Bilioni 12.12, kutoka kwa Taasisi 58 zilizotoa gawio kwa Serikali baada ya agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, alilolitoa  Novemba 24, Ikulu jijini Dodoma.
 Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, akitoa taarifa ya kiasi cha fedha ambazo zimepokelewa kutoka kwa Taasisi za Serikali ikiwa ni kuitikia agizo lililotolewa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Taasisi ambazo hazikuwasilisha gawio la Serikali Chamwino Ikulu jijini Dodoma.

 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, akisoma orodha ya Taasisi za Serikali ambazo zimetoa  gawio la Serikali kwa  Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani), jijini Dodoma.
 Sehemu ya Wawakilishi wa Taasisi waliofika kwa ajili ya kutoa gawio la Serikali wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani), wakati wa hafla ya kupokea gawio jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wenyeviti mbalimbali na Watendaji Wakuu kutoka Taasisi za Serikali baada ya halfa ya kukabidhi gawio la kiasi cha Sh. Bilioni 12.12 kutoka kwa Taasisi 58 jijini Dodoma. kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Adolf Ndunguru, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,  kulia ni Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbutuka
(Picha na Josephine Majura – WFM Dodoma).

Na Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodaoma
Serikali imesema  Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma ambazo hazitawasilisha gawio na michango yao kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali  ifikapo Januari 23 mwaka 2020, kabla ya saa 6 usiku, Bodi zitakuwa zimevunjwa na watendaji wake kupoteza ajira zao.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, wakati akipokea gawio na michango kutoka Mashirika, Kampuni na Taasisi za Umma 11, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alilolitoa Novemba 24 mwaka huu lililozitaka taasisi hizo kutoa gawio ndani ya siku 60.
Alisema itakapofika saa sita usiku ya tarehe 23 Januari, 2020 kama hawajaleta gawio wala michango ya kuingia kwenye mfuko Mkuu, Bodi hizo zimevunjwa, Watendaji Wakuu wa hizo taasisi husika nao watahusika na akabainisha kuwa hiyo ndiyo amri ya Serikali.
 “Tukio la Novemba 24, 2019 la kupokea gawio, mashirika yalikuwa 79 na Mhe. Rais, alipokea hundi ya jumla ya Sh. trillion 1.05 na aliniagiza ndani ya siku 60, Taasisi, maashirika na kampuni 187 ambazo hazikutoa gawio siku hiyo zitekeleze maagizo yake”, alieleza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa baada ya agizo la Rais, katika kipindi cha siku 18, Taasisi, Kampuni na Mashirika 58 yametekeleza agizo ambapo jumla ya fedha zilizopokelewa katika mfuko Mkuu wa Hazina ni Sh. bilioni 12.12.
Dkt. Mpango aliyapongeza mashirika, kampuni na taasisi hizo kwa kuitikia wito huo kwa kutoa fedha hizo ambazo amesema zitasaidia katika shughuli za maendeleo  ya nchi kwa njia ya ujenzi wa miradi na kuiwezesha nchi kujitegemea.
Alisema kuwa amefurahishwa na gawio na michango lakini amesema wanatakiwa kuongeza kiwango hicho mwakani kwa kuwa Watanzania wanatakiwa kuona kuwa waliopewa  dhamana  ya kusimamia mashirika yao wanatimiza wajibu wao.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbutuka, amesema idadi ndogo ya kampuni, mashirika na taasisi ya umma 71 kati ya 266 yaliyo katika orodha ya Msajili wa Hazina yaliyochangia gawio na michango mingine wakati Mhe. Rais Magufuli akipokea magawio hayo kwa niaba ya  wananchi, haikumfurahisha Kiongozi huyo wa Nchi.
Miongoni mwa Taasisi zilizotoa mchango ni pamoja na Chuo cha kilimo- SUA, Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini- IRDB, Taasisi ya Taifa ya  Usafirishaji – NIT, Mfuko wa Misitu Tanzania- TFF, Chuo cha Ufundi Stadi- VETA, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Kudhibiti ubora wa Mbegu Tanzania.
Mwisho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527