WAZIRI WA KILIMO AFANYA ZIARA YA KUSHITUKIZA KUKAGUA BEI NA UPATIKANAJI WA MBOLEA MKOANI SONGWE

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)  tarehe 21 Novemba 2019 amefanya ziara ya kushitukiza ili kujionea hali ya upatikanaji wa mbolea katika baadhi ya vijiji mkoani Songwe.

Katika ziara hiyo Mhe Hasunga kadhalika amekagua na kujionea kama wafanyabiashara wanauza mbolea kutokana na maelekezo ya serikali iliyopanga bei elekezi na kuitangaza hivi karibuni.

Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi katika kijiji na Kata ya Ipunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mhe Hasunga amempongeza mfanyabiashara wa pembejeo kijijini hapo Ndg Lukas Simkonda kwa kuuza mbolea kwa gharama ya chini kuliko bei elekezi.

“Wewe ni miongoni mwa wafanyabiashara tunaowataka, serikali imepanga bei elekezi lakini wewe umeamua kuuza chini ya bei elekezi ili kuwanufaisha zaidi wakulima, jambo hili sisi kama serikali tunaliunga mkono na kukupongeza kwa dhati kwa kazi ya kizalendo unayoifanya” Alisisitiza Mhe Hasunga

Katika hatua nyingine Wafanyabiashara wa mbolea nchini wametakiwa kuuza bidhaa hiyo kwa kufuata bei elekezi zilizotangazwa na Waziri wa Kilimo hivi karibuni kwani lengo la serikali ni kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya uhakika na kwa bei nafuu.

Aliitaja sababu ya kuwa na bei elekezi ya mbolea kuwa ni kukuza kilimo na kuongeza mavuno ya mazao ambayo ndio malighafi kuu inayohitajika wakati huu ambapo serikali inatekeleza mipango ya ukuaji wa viwanda, kama msingi mkuu wa uchumi.

Katika ziara hiyo Mhe Hasunga akiwa katika zahanati ya Ipunda katika Jimbo lake la uchaguzi la Vwawa amewapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kujitokeza kwa wingi kupima Virusi vya UKIMWI na UKIMWI kwani amesema kupima afya ni msingi wa uimarishaji wa afya zao.

Vilevile Mhe Hasunga amewataka wakulima kula chakula kizuri chenye mchanganyiko wa mbogamboga na matunda. “Wakulima wangu mnaniangusha maana ninyi mnalima na kuzalisha chakula cha kutosha lakini ajabu ninyi ndio mnaongoza kutokula vizuri jambo hili sio sahihi kabisa, mnapaswa kuimarisha afya zenu kwa kula vizuri” Alisema Mhe Hasunga

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amewapongeza wajasiriamali Wilayani Mbozi kwa kuanzisha viwanda vidogo vya ubanguaji wa karanga kwani vitaongeza uwezekano wa wakulima kuongeza uzalishaji wa karanga kwakuwai nyenzo za kubangua zitakuwepo kutokana na teknolojia hiyo ya kisasa.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ameanza ziara ya kikazi ya siku 6 mkoani humo ambapo pamoja na mambo mengine anakagua hali ya upatikanaji wa mbolea pamoja na kukagua kama wafanyabiashara wanauza mbolea kutokana na bei elekezi iliyowekwa na serikali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post