WAZIRI WA KILIMO ABAINI UBADHILIFU BODI YA KOROSHO, AUNDA TUME KUCHUNGUZA


WAZIRI wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi kwenye mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao la Korosho baada ya kubaini kuwepo na udanganyifu.

Mhe Hasunga amemuagiza CAG kuchunguza kiasi cha Shilingi Bilioni 53.2 kilichobaki kwenye akaunti ya Mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao la Korosho ambazo zilikuwa kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho na maghala.

Aidha Mhe Waziri ameunda timu ya watu wasiozidi watano kwa ajili ya kuhakiki kiasi cha korosho kilichopokelewa na kilichouzwa katika msimu wa Korosho wa mwaka 2018/2019 baada ya kubaini uwepo wa udanganyifu.

Hayo ameyasema jana tarehe 17 Novemba 2019 jijini Dodoma mbele ya wandishi wa habari ambapo amezitaka pia kamati za ulinzi na usalama kusimamia zoezi la uhakiki ambalo linaonekana kutawaliwa na udanganyifu ambapo timu iliyoundwa itashirikiana na timu iliyokuwepo chini ya wizara hiyo kuhakiki pia fedha zilizopatikana ili wahakikishe wanaolipwa ni wale wanaostahili.

Aidha amesema timu hiyo ihakikishe kuwa majina yaliyotoka kwenye vyama vya msingi kwenda kwenye vyama vikuu hadi fedha zilizoingia benki  kama kweli ziliingia kwenye akaunti za wakulima na kama kuna unyaufu uliojitokeza wabainishe ni kwa kiwango gani ili kusaidia serikali kutoa taarifa yenye uhalisia.

Waziri Hasunga amesema mwaka 2016 serikali iliamua kufuta mfuko wa Wakfu na kwenye akaunti kulikuwa na kiasi cha shilingi bilioni 53.2 lakini bodi ya Korosho iliamua kubadili matumizi na kutumia fedha hizo tofauti na maagizo yaliyotolewa na serikali.

"Kama Wizara hatupo tayari kuona ubadhilifu wowote wa fedha za umma unafanyika, Serikali ya awamu ya tano haiwezi kukubali kuona watu wachache wanafaidika na fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Timu zote mbili naziagiza hadi kufikia Januari 15 mwaka 2020 wawe wameshatuletea ripoti wizarani. Niwahakikishie hatutomvumilie yeyote ambaye atajaribu kugusa fedha za wananchi, " Amesema Waziri Hasunga.

Amesema bodi hiyo ilitumia kiasi cha shilingi bilioni 28.1 kununua viuatilifu,walitumia kiasi cha shilingi bilioni 12.2 kulipia magunia ilhali katika msimu huo wanunuzi walikuwa wananunua magunia wao wenyewe.

Ametoa wito kwa wakulima kuwa kama kuna anayedai ushirika apelike madai yao kwenye kamati ya ulinzi na usalama na timu iliyoundwa ili waseme kama hawajalipwa.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post