MWANAMKE AKAMATWA NA KADI 23 ZA BENKI AKIWA AMEZIFICHA KWENYE SEHEMU ZAKE ZA SIRI DAR

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Halima Juma (23), mkazi wa Chalinze mkoani Pwani, baada ya kudaiwa kukutwa na kadi za ATM 23 alizozificha sehemu za siri.

Imedaiwa na jeshi hilo kuwa alikuwa anazitumia kuiba fedha katika benki mbalimbali nchini kwa kujitolea kuwapa msaada watu wasiojua kutumia kadi za ATM, baadaye kuwabadilishia kadi zao kinyemela.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alidai mbele ya waandishi wa habari jijini jana kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumanne kwenye tawi la Benki ya CRDB Mbagala wilayani Temeke.

“Askari wetu walimtilia shaka binti huyu ambaye wakati huo alikuwa katika chumba cha ATM cha CRDB akijifanya anawasaidia wazee na wastaafu wasiojua kutumia mashine hizo.

“Lengo lake lilikuwa ni kuchukua namba za siri zao kisha kuwabadilishia kadi za ATM na baadaye kuwaibia fedha kwenye akaunti zao kwa kutumia kadi halisi za wahusika baada ya kuzibadilisha 'password' (nywila),” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na askari wanaolinda benki hiyo na alipopekuliwa katika pochi yake aliyoificha sehemu za siri, alikutwa na kadi za ATM 23 za watu mbalimbali.

“Alikutwa na kadi saba za CRDB, sita za NMB na benki za NBC, Amana na Posta, ambazo alikutwa na kadi mbili mbili kwa hizo benki zingine. Pia alikutwa na kadi moja moja za benki za ACB, Stanbic, DTB na Equity," alidai.

Kamanda Mambosasa alidai mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na jeshi hilo na atafikishwa mahakamani wakati wowote.

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM KUIMARISHA ULINZI KATIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limejipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa amani na utulivu.




Ndugu wana habari, tarehe 24/11/2019 ni siku ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji hivyo basi sisi kama Jeshi la Polisi tutaimarisha ulinzi maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam, katika vituo vya kupigia kura, ofisi zote za vyama vya siasa na ofisi zote za watendaji wa kata.

Aidha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi chochote cha watu watakao jaribu kuvuruga amani jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA WIZI WA FEDHA KWENYE MASHINE ZA KUTOLEA FEDHA (ATM) NA ATM KADI 23
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Bi Halima Juma (23)Mkazi wa Chalinze kwa tuhuma za wizi wa fedha kwenye mashine za kutolea fedha (ATM)

Mnamo tarehe 19/11/2019 katika benki ya CRDB tawi la Mbagala akiwa katika ATM hizo, aidha alimtilia mashaka binti huyo aliyekuwa kwenye chumba cha ATM ya benki hiyo akijifanya kuwasaidia wazee na wastaafu wasiojua kutumia ATM mashine vizuri, lakini lengo lake ni kuchukua namba za siri za wastaafu na wazee hao na kisha kuwabadilishia ATM kadi zao na baadaye kuwaibia fedha kwenye akaunti zao kwa kutumia kadi halisi za wahusika baada ya kuwabadilishia kadi na kuchukua namba za siri.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na askari wanaolinda Benki hiyo na alipopekuliwa alikutwa na ATM kadi 23 za watu mbalimbali za benki tofauti tofauti zikiwa katika pochi yake huku akiwa amezificha katika sehemu zake za siri ukeni.

Kadi hizo ni kama ifuatavyo;
1.CRDB kadi 07
2.NMB kadi 06
3.NBC kadi 02
4.AMANA kadi 02
5.POSTA BENKI kadi 02
6.ACB kadi 01
7.STANIBIC kadi 01
8.DTB kadi 01
9.EQUITY kadi 01

Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani hivi karibuni.

TAHADHARI YA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES SALAAM.​

Jeshi la Polisi kanda maalum Dar es salaam linapenda kutoa tahadhari kwa wakazi wa jiji la Dsm wote kuwa makini kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepukana na majanga yanayoweza kuepukika. 

Hivyo wananchi wote wanatakiwa kuwa makini na watoto wadogo wanaohitaji uangalizi wa karibu, pia kujiepusha kupita kwenye maji ya mito midogomidogo au madimbwi ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.

Aidha hadi sasa zimepokelewa taarifa za watu wawili kufariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

LAZARO .B. MAMBOSASA – SACP
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAM.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527