TAKUKURU GEITA YAWAKAMATA VIONGOZI WA AMCOS WALIOTAFUNA FEDHA ZA WAKULIMA


NA SALVATORY NTANDU
Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani wa Geita imefanikiwa  kurejesha shilingi milioni 23 kati ya 49 zilizokuwa zimeibwa na baadhi ya  viongozi wa vyama vya Ushiriaka (AMCOS) 8 katika wilaya Mbogwe.

Kauli hiyo imetolewa jana na Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Geita, Leonidas Felix katika hafla maalumu ya kukabidhi shilingi milioni 15 kwa wakulima wa chama cha ushirika Mwanza madaso zilizorudishwa na baadhi ya viongozi wa AMCOMS hizo.

Amesema TAKUKURU iliendesha zoezi la ukaguzi katika AMCOS zote katika mkoa wa Geita na kubaini baadhi ya viongozi wake kutumia fedha za wakulima wa zao la pamba kujinufaisha wao na kutowalipa kwa kuwahadaa kuwa kampuni za ununuzi bado hazijalipa licha ya kuwa wao tayari wameshalipwa.

“Mpaka sasa tunawashikilia viongozi 22 wa AMCOS mbalimbali katika mkoa wetu ambao wameiba fedha za wakulima tumewapa wiki mmoja tuu kurejesha fedha hizo wengine tayari wameanza kutiii agizo hili na kurejesha shilingi milioni 23”alisema Felix.

Amefafanua kuwa katika zoezi la ufuatiliaji wa madeni ya wakulima wa zao la pamba katika mkoa huo wamebaini baadhi ya kampuni za ununuzi wa zao la pamba kutowalipa wakulima ambapo katika halmashauri ya wilaya ya  Geita wakulima wanadai zaidi ya shilingi bilioni 1 ambazo wanapaswa kuzilipa kwa muda wa wiki mmoja ili kuwawezesha kujiandaa na msimu mpya wa kilimo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya Mbogwe,  Matha Mkupas  amewataka viongozi wa AMCOS kwa kushirikiana na Maafisa Ushirika kuhakikisha wakulima wanalipa madeni ya pembejeo ya msimu uliopita kabla ya kulipwa fedha zao  baada ya kampuni za ununuzi wa pamba kuwalipa.

“serikali ya awamu ya Tano haiwezi kukubali wakulima wake kuendelea kunyanyaswa na viongozi wa AMCOS ambao ni wabadhilifu wanaowaibia wakulima tutahakikisha tunawakamata wote hadi walipe fedha za wakulima”alisema Mkupas.

Nao baadhi ya wakulima wa Zao la Pamba katika AMCOS ya Mwanza Madaso, Suzana Nkinjiwa na Rafael Shizya wamesema kucheleweshwa kwa malipo ya zao hilo kwa msimu huu yatasababisha kushuka kwa uzalishaji kutokana na wakulima wengi kukata tamaa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527