POLEPOLE: CCM IMEJIPANGA VIZURI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Na Ahmed Mahmoud,Arusha

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM),kimesema kuwa kimejipanga kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika novemba 24 mwaka huu na kimewaonya wale wote ambao wamepanga kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kuacha mara moja kuchochea wananchi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa,Humphrey Polepole alitoa kauli hiyo Novemba 17 jijini Arusha alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya CCM Mkoa wa Arusha na kueleza kuwa ushindi wa kishindo wanaotarajia kuupata ni kutokana na wananchi kuridhishwa na utendaji wa serikali ya awamu ya tano.

Amevitaka vyama vyama vya upinzani kuheshimu kanuni,sheria na taratibu za uchaguzi na kwamba wasipange au wasiwashawishi wafuasi wao kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wote kuanzia kipindi cha kampeni,upigaji kura,kuhesabu matokeo pamoja na kutangazwa kwa mshindi kwa kuwa chama hicho kimejipanga kikamilifu.

“Wananchi wameridhishwa na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwani katika kipindi cha miaka mine ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano miradi mingi ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya mwananchi wa kawaida imetekelezwa kwa kiwango kikubwa sana”alisema.

Polepole aliitaja baadhi ya miradi ambayo imetekelezwa kwa kiwango kikubwa katika kipindi kifupi cha miaka mine kuwa ni ujenzi wa vituo vya afya na hosipitali za Wilaya,upatikanaji wa maji safi na salama,ujenzi wa barabara na madaraja,usambazaji wa umeme katika maeneo mengi ya mijini na vijijini,ujenzi wa vyumba wa madarasa,nyumba za walimu pamoja na maabara.

Alisema kuwa mkutano huo na wanahabari ni matokeo ya kikao kazi cha kufanya tathmini ya kimaendeleo ya miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli na kueleza kuwa Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa hapa nchini ambayo miradi mingi ya kimaendeleo imetekelezwa.

Alisema kuwa wimbi la wananchama waliotoka kwenda vyama vya upinzani mara baada ya mzee na Waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa kuhamia huko ndio lililopelekea chama hicho kuanza kujitathmini na kuandaa mikakati ya ushindi ikiwemo kurudi nyumbani kwa kiongozi huyo kumekisaidia chama hicho kuvuna wanachama wengi zaidi kwa kipindi kifupi.

Alisema kuwa mkutano huo na wanahabari ni matokeo ya kikao kazi cha kufanya tathmini ya kimaendeleo ya miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli na kueleza kuwa Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa hapa nchini ambayo miradi mingi ya kimaendeleo imetekelezwa.

Kadhalika katibu huyo wa Itikadi na uenezi alieleza kushangazwa kwake na baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vimetangaza kujitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kueleza kuwa baadhi ya vyama vilivyotangaza kujitoa havikuwahi kusimamisha mgombea hata mmoja na kuhoji wanajitoa wapi.

Awali akimkaribisha Katibu huyo wa Itikadi na uenezi Taifa,Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha,Mussa Matoroka alisema kuwa kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa CCM Mkoa wa Arusha imejipanga kikamilifu, kimkakati na kisayansi  kwa kuhakikisha kuwa wanashinda kwa kishido katika uchaguzi huo.

Aliwataka wananchi wa mkoani hapa kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kutimiza haki yao ya msingi kikatiba ya kuchagua katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa kwa ajili ya kufanyika kwa uchaguzi huo ambapo pia amewasishi kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kabla na baada ya uchaguzi.

Katika mkutano huo katibu huo wa Itikadi na uenezi taifa aliambatana na viongozi mbalimbali wa chama hicho ngazi ya Mkoa na Wilaya ambapo kila mmoja alipata fursa ya kuzunguza juu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika eneo lake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527