














Na Mwandishi Wetu.
Afrika haitaweza kupiga hatua endapo itaendelea kuwa muuzaji wa bidhaa ghafi na muagizaji wa bidhaa za viwandani.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Joseph Magufuli wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za Afrika na Nordic unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema kuwa kwa sasa, asilimia 60 ya mauzo ya nje kutoka nchi za Afrika ni mazao ghafi hivyo ni lazima Waafrika tufike hatua ambapo tutaweza kusindika na kuongeza thamani ya mazao yetu, ikiwemo mazao ya kilimo, madini, uvuvi, nk.
“Tunataka tusindike pamba na kutengeneza nguo hapa Afrika; tunataka tuchimbe madini na kuyachenjua hapa hapa Afrika; tunataka tuvue samaki na kuwasindika hapa hapa Afrika.
Africa must produce, process, consume and export finished products,” amesema.
Ameongeza kuwa Viwanda ni moja ya vipaumbele vyetu vikubwa, na washirika wetu wa maendeleo pamoja na wawekezaji wengine makini watuunge mkono kwenye mwelekeo huo.
Amesema kwa kuwa nchi marafiki za Nordic wamepiga hatua kiteknolojia, hususan teknolojia ya viwanda, tushirikiane kujenga viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao yetu kwa manufaa ya pande zetu mbili.
Vile vile ameosema ili kuweza ili kuvutia biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali, ni muhimu kwa nchi za Afrika kuweka mazingira muafaka, ikiwemo miundombinu wezeshi pamoja na kuondoa urasimu kwenye sheria na taratibu zetu za biashara na uwekezaji.
Amesema mpaka sasa Tanzania imefanikiwa kupitia na kurekebisha sheria na taratibu mbalimbali za uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na kutengeneza sheria za kuwalinda wawekezaji.
“Tumeanzisha Wizara mahsusi yenye dhamana ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili ijihusishe moja kwa moja na kurahisisha mazingira na uratibu wa uwekezaji nchini,” amesema.
Lakini muhimu zaidi, tunatekeleza Mkakati wa Kurekebisha na Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini, yaani The Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Environment.
Amesema jitihada zingine ni kutenga kanda maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na kanda maalumu za uwekezaji, yaani Export Processing Zones and Special Economic Zones. Sambamba na hayo, Tanzania kutambua umuhimu wa miundombinu wezeshi kama kichocheo cha biashara na uwekezaji, hivi sasa, inajenga na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo barabara, reli, usafiri wa majini na anga.
Amesema hivi sasa wanajenga Reli ya Kisasa, yaani Standard Gauge Railway kwenye Ushoroba wa Kati yenye urefu wa kilomita 1,800 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, ambayo baadaye itaunganisha na nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Ameongeza kuwa ili kuvutia wawekezaji wameza kulifufua Shirika letu la Ndege la ATCL na kuboresha viwanja vyetu vya ndege na kusimika rada za kuongozea ndege ikiwemo kupanua na kuboresha bandari zetu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga pamoja zilizopo kwenye Maziwa yetu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Amesema upanuzi huu umeenda sambamba na ujenzi wa meli na vivuko. Zaidi ya hapo, tutakeleza Mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme wa maji kwenye Bonde la Rufiji utakaozalisha Megawati 2,115, na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa viwandani na kwenye sekta nyingine.
Amemalizia kwa kuzikaribisha nchi za Nordic, pamoja na mataifa mengine, yakiwemo ya Afrika, kuja kuwekeza nchini Tanzania ambapo kuna mazingira wezeshi ya uwekezaji ni muafaka na yanatabirika, kutokana na amani na utulivu wa kisiasa, lakini pia mwenendo wa ukuaji wa uchumi ni mzuri ambapo, kwa sasa, ni wastani wa asilimia 7.
Zaidi ya hapo, Tanzania ni wanachama wa SADC na EAC, ambazo kwa pamoja zina idadi ya watu wapatao milioni 450.
Social Plugin