KATIBU MKUU TAMISEMI ATAKA SHERIA, KANUNI NA MIONGOZO YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA WA MWAKA 2019 ZIFUATWE


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka viongozi na wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa karibu Kanuni, Sheria, na Miongozo mbalimbali iliyowekwa ili uchaguzi huo ufanyike katika mazingira ya amani na uwe huru na haki.

Katibu Mkuu ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akielezea hatua inayofuata baada ya zoezi la uchukuaji na urejeshwaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kukamilika hapo jana ambapo amesema zoezi linaloendelea kwa tarehe 5 Novemba, 2019 ni Uteuzi wa Wagombea katika nafasi za Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa na nafasi ya Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa.

Amesema kuwa kuanzia tarehe 5 hadi 6 Novemba, 2019 ni kipindi cha watu walioomba kuteuliwa kuwa wagombea au wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ambao hawajaridhika na uteuzi uliofanywa na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuwasilisha pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea.

 “Nitoe maelekezo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kusimamia kwa weledi zoezi la uwasilishaji wa pingamizi na kutoa uamuzi wa haki kuhusu pingamizi hizo za uteuzi wa wagombea” amesisitiza Katibu mkuu.

Mhandisi Nyamhanga ameseama kwamba baada ya Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kupokea pingamizi na kutoa uamuzi, waombaji au wagombea ambao hawataridhika na uamuzi wa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi watakuwa na haki ya kukata rufaa kati ya tarehe 5 hadi 8 Novemba,  2019 kwenye Kamati za Rufani zilizoanzishwa katika kila Wilaya nchini.

Aidha, Kamati za Rufani zitatoa uamuzi kuhusu rufaa mbalimbali zilizowasilishwa kwake kati ya tarehe 5 na 9 Novemba, 2019.  Vilevile, mtu yeyote ambaye ameomba kuteuliwa kuwa mgombea au mgombea ambaye hajaridhika na uamuzi wa Kamati ya Rufani atakuwa na haki ya kufungua kesi katika Mahakama ya Wilaya ndani ya muda wa siku 30 baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Mhandisi Nyamhanga amevikumbusha Vyama vya Siasa ambavyo vitashiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 kuhakikisha vinawasilisha ratiba za mikutano ya kampeni kwa Wasimamizi wa Uchaguzi tarehe 10 Novemba, 2019 kama ilivyooneshwa kwenye ratiba ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527