AFARIKI KWA KUFYATUKIWA RISASI ILIYOBEBWA NA MWENZAKE KATAVI

Na Walter Mguluchuma -Malunde1 blog Katavi
Mkazi wa kijiji cha Magula, Kata ya Machimboni,tarafa ya Nsimbo wilayani Mpanda mkoa wa Katavi,Masood Mtegitwe(27) anayedhaniwa kuwa ni jambazi amefariki dunia baada ya risasi kufyatuka kutoka kwenye bunduki ya kivita aliyokuwa ameibeba mwenzake ambaye naye anadhaniwa ni jambazi kutokana na kutokuwa na utaalamu wa kubeba silaha.

Tukio hilo limetokea Novemba 11 majira ya saa 3 :00 usiku wakati watu hao wakiwa wanatembea kijijini wakiwa na mfuko wa aina ya sulphate uliyokuwa na silaha ndani yake aina ya AK 47 yenye namba TX 4039, magazini moja yenye risasi tisa, ganda moja la risasi na kofia ngumu ya pikipiki helmet.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Benjamin Kuzaga alisema watu hao walikuwa wanakwenda kusikojulikana wakiwa wamebeba bunduki hiyo kwenye mfuko, ndipo risasi zilipofyatuka na kumuua mwenzake.

Kamanda huyo alisema baada ya mwenzake kujua kuwa Masood Mtegitwe amefariki dunia alitokomea kusikojulikana kwa kutumia usafiri wa pikipiki ambayo haijafahamika ni mali ya nani kwa kuwa haikukutwa kwenye eneo la tukio.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo wananchi walifika kwenye eneo hilo na walikuta amefariki dunia na walitoa taarifa kwa jeshi la polisi ambao walifika kwenye eneo hilo na baada ya kufanya ukaguzi wao walipata silaha hiyo ya kivita ikiwa na magazini moja yenye risasi sita,ganda moja la risasi na kofia ngumu ya pikipiki.

Kamanda huyo wa polisi alisema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa,kwani katika upelelezi wa awali inaonyesha watu hao walikuwa majambazi na hakuna mtu aliyekamatwa kufuatia tukio hilo.

Alisema upelelezi na msako mkali unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi wa eneo husika ili kuhakikisha kuwa mtu aliyekuwa na marehemu anapatikana ili afikishwe mahakamani akajibu tuhuma zitakazomkabili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post