HAKIMU WA KABENDERA ATEULIWA KUWA JAJI WA MAHAKAMA KUU ,KESI YAPIGWA KALENDA


Kesi inayomkabili Mwandishi wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera, imesogezwa mbele hadi Novemba 20, 2019, baada ya Hakimu Augustine Rwizile, aliyekuwa akiisikiliza kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, ambapo kwa sasa kesi hiyo inasubiri kupangiwa Hakimu mwingine.

Akizungumza mahakamani hapo leo Novemba 7, 2019, Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mkazi Vicky Mwaikambo, amesema kuwa kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la utakatishaji wa fedha zaidi ya Shilingi milioni 173, uhujumu uchumi na ukwepaji wa kodi.


Katika shtaka la kwanza, Kabendera anadaiwa kuwa alijihusisha na mtandao wa kihalifu kwa kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Shtaka la pili anadaiwa kuwa bila sababu, alikwepa kodi ya Sh173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la tatu, Kabendera anadaiwa kutakaisha Sh173,247047.02 huku akijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu na utakatishaji fedha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527