SERIKALI YAANZA MCHAKATO WA KUPANDIKIZA FARU WEUPE NCHINI KWA MARA YA KWANZA


Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Khamis Kigwangala  akiwa na baadhi ya wasanii wa muziki na filamu katika hifadhi ya Burigi Chato

Na Ashura Jumapili - Malunde 1 blog 

WIZARA ya Maliasili na Utalii ipo katika mchakato wa kupandikiza Wanyama zaidi wa aina mbalimbali katika hifadhi mpya ya Taifa ya Burigi Chato wakiwemo Faru weupe ili iweze kuwa kivutio kwa watalii mbalimbali ambao wameanza kutembelea hifadhi hiyo.

Akiongoza zoezi la utalii wa kutembea kwa miguu akiwa amefuatana na wasanii wa muziki na filamu katika hifadhi hiyo, mpya iliyopo katika mikoa ya Kagera na Chato Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Khamis Kigwangala amesema kwa mara ya kwanza Serikali ya Tanzania imeamua kupandikiza Faru weupe katika hifadhi ya Burigi Chato.

Alisema utatifi bado unaendelea wa kuangalia namna ambavyo Faru hao weupe wataweza kuishi katika hifadhi hiyo kwa sababu hawakuwahi kuwepo kabisa hapa nchini.

Alisema ,Asili ya Faru weupe wanazaliana kwa wingi na kwa haraka hivyo wakipandikizwa katika hifadhi hiyo watasaidia sana kukuza idadi ya Faru weupe katika nchi na pia kuendelea kuwahifadhi kwa faida ya dunia nzima.

Pia alisema utafiti wa kupandikiza Faru weusi katika hifadhi hiyo umekamilika na malisho yapo ya kutosha na kudai kuwa asili ya hifadhi ya Burigi Chato ni nchi ya Faru historia inaonyesha kulikuwa na Faru wengi.

Alisema pia wamesha peleka familia moja ya Simba kutoka hifadhi ya Serengeti Mkoani Mara na kudai kuwa bado wapo kwenye uzio na wataachiwa rasmi baada ya wiki mbili.

 Msanii wa filamu Steven Mengele maarufu kama (Steve Nyerere) alisema hifadhi ya Burigi Chato ilichelewa sana lakini awamu ya tano imewekezekana chini ya msimamizi wake Khamis Kigwangala na wizara nzima ya maliasili na utalii.

Mengele,alisema Burigi Chato ndio mbuga ya kwanza yenye Twiga warefu na weusi pia ina kila vivutio alivyowahi kuviona.

Single Mtamabile,maarufu kama (Rich )alisema kutembelea hifadhi unapata uzoefu mkubwa sana katika mambo ya uhifadhi wa mazingira na utalii.

“Sisi wenyewe tulikuwa tunaona ni kawaida lakini tulipofika katika hifadhi hii ya Burigi Chato tumeona na kujifunza vitu vingi katika masuala ya Utalii”,alisema Mtambalike.

Alisema kujenga tabia ya kutembelea hifadhi za Taifa unakuwa unalinda asili yako na rasiliamali za nchi kwa kufika kujifunza na kuelewa namna ya kuendelea kutunza na kuhifadhi mazingira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post