TAIFA STARS YAANZA VYEMA MBIO ZA AFCON 2021, YAICHAPA EQUATORIAL GUINEA 2-1


Tanzania imeanza vyema mbio za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021 baada ya kutoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Equatorial Guinea usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Haukuwa ushindi mwepesi, kwani hadi mapumziko, tayari Equatorial Guinea walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa Sassuolo ya Italia, Pedro Mba Obiang dakika ya 15 akimtungua kipa mkongwe wa Tanzania, Juma Kaseja kwa shuti la mbali.

Mshambuliaji huyo zamani wa West Ham United ya England aliendelea kulitia majaribu lango la Taifa Stars, lakini safu ya ulinzi ilisimama imara kutompa nafasi nyingine.

Dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili, kocha Mrundi wa Tanzania, Etienne Ndayiragijje alianza na mabadiliko ya kuongeza nguvu katika safu ys ushambuliaji, akimtoa beki wa kulia Hassan Ramadhani Kessy na kumuingiza mshambuliaji, Ditram Nchimbi.

Ni mabadiliko hayo yaliyoisaidia Taifa Stars kupata bao la kusawazisha likifungwa na kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happygod Msuva dakika ya 68 akimalizia mpira uliookolewa na kipa baaada ya yeye mwenyewe kuunganisha kwa kichwa kona ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Taifa Stars iliongeza kasi ya mashambulizi baada ya bao hilo na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 90 na ushei baada ya kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar Junior ‘Sure Boy’ kufunga bao la ushindi kwa shuti la mbali. 

Baada ya ushindi huo, Taifa Stars itasafiri kuwafuata Libya Uwanja wa Mustapha Ben Jannet mjini Monastir Jumanne ya Novemba 19 kwa mchezo wa pili wa kundi hilo.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Juma Kaseja, Hassan Kessy/Ditram Nchimbi dk50, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kelvin Yondan, Bakari Nondo, Erasto Nyoni, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Muzamil Yassin, Simon Msuva, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Hassan Dilunga dk75.

Equatorial Guinea; Felipe Ovono Ovono, Igor Engonga Noval, Carlos Akapo Martinez, Basilio Ndong Nchama, Esteban Orozco, Jose Machin/Yannick Bulya Sam dk65, Pablo Ganet, Pedro Mba Obiang, Ruben Belima/Federico Akieme dk77, Enrique Kike Boula/Pedro Oba Mbengono Asu dk71 na Emilio Nsué Lopez.
Chanzo - Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post