DIWANI AJITOLEA KULIPIA JENGO LITUMIKE KAMA OFISI YA KUSIKILIZA KERO ZA WAZEE

Diwani wa Kata ya Izigo Edwin Njunwa
Na Lydia Lugakila -Malunde 1 blog
Diwani wa Kata ya Izigo Wilayani Muleba mkoani Kagera Edwin Njunwa amejitolea  kulipia miezi 6 kodi ya jengo lililopo kwenye kata hiyo liwe ofisi ya kuhudumia wananchi hususani kutatua kero za wazee kutokana na wazee kufuata ofisi umbali mrefu.

Ahadi hiyo imetolewa na diwani huyo Edwin Njunwa Oktoba mosi 2019,katika maadhimisho ya siku ya wazeee duniani iliyofanyikaa wilayani humo.

Njunwa amesema ameamua kujitolea kulipia jengo hilo ili kuunga jitihada za rais Magufuli kutokana na kuwajali, kuwalinda na kuwatetea wanyonge hususani wazee kwani wazee katika kata hiyo wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu kufuata ofisi ya kutatua kero zao umbali mrefu jambo ambalo huwa gumu kwa wazee hao na kushindwa kupata stahiki zao ipasavyo.

Diwani huyo amemuomba mkuu wa wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Luyango kuwa karibu na ofisi hiyo kwa kushiriki kuizindua na baadaye kuitembelea mara kwa mara ili kuyasikiliza matakwa ya wazee hao na kuwapatia msaada wa haraka pale wanapokumbana na changamoto katika jamii.

"Mheshimiwa mkuu wa wilaya, mimi kama diwani nimejitolea ofisi ya wazee kata ya Izigo kwa kulipia jengo ambalo lililopo hapa na wewe kama mkuu wangu ninayeamini utendaji kazi wako unaoendana na kasi ya Rais Magufuli ninaamini na utakuwa mchango mkubwa kwa wazeee hawa’’,alisema diwani huyo.

Diwani Njunwa amesema katika juhudi zake amefanikiwa kupata kampuni ambayo imejitolea kutoa huduma moja kwa mwezi ili kutoa msaada wa huduma ya kisheria kwa wazee hao.

Naye mkuu wa wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Luyango amejitolea vifaa mbalimbali vya kuanzia katika ofisi hiyo mpya ikiwemo viti,na meza.

"Natambua sana wazee kwa kuwa kila wiki nimekuwa na utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi ikiwa ni pamoja na nyie wazeee kwa hiyo nipo bega kwa bega",alisema mkuu wa wilaya hiyo

Hata hiyo mkuu huyo wa wilaya amewataka wazee hao kupaza sauti zao katika ofisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa ili kukomesha vitendo vya rushwa vinavyowafanya wazee wao kuendelea kupata changamoto kutokana na watu wasio wema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527