WAUGUZI WAOMBA WAPUNGUZIWE ADA ZA LESENI ZA UUGUZI

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Wauguzi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara wameomba Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini(TNMC) kupunguza  gharama za ada ya leseni za uuguzi ambazo wamedai kuwa ni kubwa na zinaathiri vipato vyao.

Ombi hilo limetolewa na Katibu wa Chama cha wauguzi Tanzania Bara(TANNA) Bw. Sebastian Luziga wakati akisoma risala mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka alipofungua Kongamano la kisayansi na Mkutano wa 47 wa wauguzi kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Oktoba 01, 2019 Mjini Bariadi.

Luziga amesema awali ada hiyo kwa ngazi ya astashahada ilikuwa 20,000/=  stashahada na shahada na shahada ya uzamili  ilikuwa shilingi 40,000/=, hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la ada ambapo astashahada wanapaswa kulipa shilingi 40,000/=, stashada 60,000/=shahada 80,000 na shahada ya uzamili na uzamivu ni 120,000/=.

“Ongezeko hili ni kubwa na linaathiri sana kipato cha wauguzi  kwani hakuna uwiano kati ya kupanda huko kwa ada na ongezeko la mshahara; kupitia Wizara ya Afya tunaomba lishughulikiwe upya kwa kufuata utaratibu wa kushirikisha wadau,” alisema Luziga

Akizungumza mara baada ya kupokea risala hiyo Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameahidi kulifikisha suala hilo pamoja na mengine yaliyowasilishwa kwa Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, huku akiwaomba viongozi kulitafakari kwa upya ongezeko la ada wakizingatia hali halisi ya mishahara ya wauguzi, kodi na makato na waone busara kama ipo haja na hoja ya kuongeza ada hiyo.

“Suala hili ni hoja ya walio wengi, ninyi nyote mmemuona Mhe. Rais akizungumzia kuondolewa kwa tozo nyingi zisizo na sababu kwenye kilimo, mifugo, uvuvi; hata hili la kwenu linaweza kusababisha serikali iwe na nia ya kufahamu mabaraza yake yote na tozo zao, nawaomba viongozi mlitafakari muone kama ipo hoja na haja ya kuongeza gharama za ada,” alisema Mtaka.

Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt. Festo Dugange amesema mkoa unatambua kazi inayofanywa na wauguzi  ya kutoa elimu kwa wajawazito na kuhamasisha wajifungulie  kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo mwaka 2017 wanawake waliojifungulia kwenye vituo vya afya ni asilimia 55 na mwaka 2018 ikapanda kufikia  asilimia 70.

Naye Afisa Muuguzi kutoka Halmashauri ya Ubungo Bi. Aliho Ngeregenza amesema  wauguzi walio wengi vipato vyao wanavyopata haviendani na gharama za leseni wanazolipia hivyo ombi lao wapunguziwe gharama hizo

Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 47 wa wauguzi Tanzania Bara ambalo linahusisha wauguzi zaidi ya 800 litafanyika kwa muda wa siku nne Mjini Bariadi mkoani Simiyu.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527