KAILIMA: WATUMISHI WA UMMA, WATANZANIA JITOKEZENI KUJIANDIKISHA

Na Mwandishi Wetu, MOHA
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhan Kailima, ametoa wito kwa watumishi wa umma na Watanzania kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kutumia fursa hiyo kuchague viongozi wenye sifa karika  Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

 
Kailima aliyasema hayo Mjini Dodoma jana asubuhi baada ya  kujiandikisha katika daftari hilo kwenye kituo kilichopo Mtaa wa Chimuli, Kata ya Makole.

Alisema uzoefu unaonyesha kuwa, kuna mwamko mdogo kwa kundi la watumishi wa umma kujiandikisha, kushiriki uchaguzi huo ili waweze kuchagua viongozi wenye sifa.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla, uandikishaji huu umeanza Oktoba 8-14, mwaka huu.

“Kampeni zitafanyika kwa wiki moja kuanzia Novemba 17-23, mwaka huu, uchaguzi utafanyika Novemba 24, mwaka huu…ni muhimu jamii kutambua kuwa, mshindi katika uchaguzi huu atapatikana kwa idadi ya wapiga kura sio asilimia,” alisema.

Kailima alisema ni muhimu Watanzania wakashiriki uchaguzi huo uli watumie fursa hiyo kuchagua kiongozi anayestahili, wasiposhiriki atachaguliwa Mwenyekiti wa Serikali ama mjumbe ambaye jamii kubwa haitapenda achaguliwe.

“Nawaomba wananchi wahudhurie kampeni, waulize maswali kwa wagombea, watumie fursa hiyo kuchagua viongozi ambao ni waadilifu na waaminifu.

“Rushwa ni adui wa maendeleo, wananchi mjiepushe kupokea rushwa, Wizara yangu kupitia taasisi zake za ulinzi na usalama ziko imara, tutaimarisha ulinzi wakati wa kampeni, upigaji kura na utangazaji matokeo,” alifafanua.

Aliwapongeza waandikishaji, wasimamizi wa zoezi hilo kwa kufika mapema kwenye vituo vya uandikishaji wapiga kura.

Alisema vituo hivyo viko sehemu barabarani, mitaani ambapo uandikishaji huo hauna vikwazo kwani hauhitaji kitambulisho cha uraia, cheti cha kuzaliwa.

“Ukifika kituoni utaulizwa majina yako kamili, umri wako, eneo unaloishi…kama eneo lako la kujiandikisha sio hilo utaelekezwa eneo la kwenda kujiandikisha,” aliongeza.

Kwa upande wao, mwandikishaji wapiga kura katika kituo hicho, Peter Ititi na mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, John Fundi walimshukuru Kailima kwa wito alioutoa ili jamii ione umuhimu wa kushiriki uchaguzi huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527