WACHINA WAAMRIWA KULIPA MILIONI 70 BAADA YA KUKIRI MAKOSA YAO IKIWEMO LA KUSAFIRISHA KUCHA ZA SIMBA


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Raia wawili wa China, Li Ling na Chen Guo kulipa faini ya Sh.Mil 70 baada ya kukiri makosa yao ikiwemo la kusafirisha Kucha 25 za Simba.

Pamoja na kuachiwa huru, mahakama hiyo imetaifisha gari aina ya Toyota Prado T 982 CDH na mashine mbili za washtakiwa hao na kuwa mali ya Serikali huku ikimtaka mshtakiwa Chen Guo kulipa faini ya Sh. Milioni 1 kwa kosa la kuishi nchini bila kibali.

Hatua hiyo, imekuja baada ya upande wa mashtaka kuwafutia washtakiwa hao mashtaka ya uhujumu uchumi na kuwasomea mashtaka mawili ya kujihusisha na nyara za serikali na kuishi nchini bila kibali.

Hata hivyo washtakiwa wengine wanne waliokuwa katika kesi hiyo ambao ni raia wa China wamegoma kukiri mashtaka yao yanayowakabili hivyo wamerudishwa rumande.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo amesema mshtakiwa Li Ling anapaswa kulipa fidia ya Sh. Mil 45 na mshtakiwa Chen Guo atalipa Sh. Mil 25 na faini ya Sh. Milioni 1 au kwenda jela mwaka mmoja.

Pia amesema, gari aina ya Toyota Prado na mashine mbili zinataifishwa na kuwa mali ya Serikali na amewataka washtakiwa hao kuondoka nchini mara moja kwa kuwa sio raia wa Tanzania. .

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Salim Msemo alidai hawana kumbukumbu ya nyuma ya makosa kwa washtakiwa hivyo, anaiomba mahakama itoe adhabu kulingana na makubaliano ili iwe fundisho kwao na wengine.

Mapema, akisoma makubaliano hayo, Wakili Msemo alidai kuwa wameingia makubaliano na washtakiwa hao baada ya kukiri kosa la kujihusisha na nyara za serikali na kuishi nchini bila kibali, hivyo wameamua kuondoa mashtaka ya uhujumu uchumi.

Baada ya kusoma makubaliano hayo, Hakimu Shaidi aliwaapisha washtakiwa na kuwauliza kama walisaini kwa hiari yao na kudai alifanya hivyo kwa hiari yao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527