VIGOGO 9 NSSF KORTINI KWA KUTAKATISHA BILIONI 2


Vigogo tisa wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Jamila Vulu, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi, wizi na kutakatisha zaidi ya Sh. bilioni mbili.

Washtakiwa hao walisomewa jana mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Kelvin Mhina katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon, aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni mwandishi wa hundi, Abdul Njozi; Meneja Uhakiki, Amir Kapera; Mhasibu James Oigo, Mhasibu Mkuu, Hellen Peter na Mhasibu Mwandamizi anayeshughulikia matumizi, Ivonne Kimaro.

Wengine ni Kaimu Meneja Rasilimali Watu, Tikyeba Alphonce na Mhasibu Dominic Mbwete.

Akisoma hati ya mashtaka hayo, Wankyo Simon alidai  kati ya Julai Mosi, 2016 na Septemba 4, 2017 maeneo Dar es Salaam washtakiwa hao pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani  walikula njama na kutakatisha fedha kiasi cha zaidi ya Sh2 bilioni wakiharibu kuonyesha hundi hizo halali zimetolewa na bodi ya wadhamini ya NSSF huku wakijua si kweli.


Katika shtaka la pili kati ya Julai Mosi, 2016 na Septemba 4, 2017 wakiwa katika ofisi za NSSF makao makuu iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa Njozi na Kapera kwa nia ya kufanya udanganyifu walighushi jumla ya hundi 47 za benki ya CRDB ambazo ni akaunti namba 01J1028249500 ya bodi ya wadhamini ya NSSF.



Shitaka la tatu tarehe hiyo katika ofisi za NSSF makao makuu iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam washtakiwa wote wakiwa watumishi wa umma walioajiliwa waiiba zaidi ya Sh2 bilioni mali ya bodi ya wadhamini ya NSSF.



Simon alidai katika shtaka la nne tarehe hiyo hiyo katika ofisi za NSSF makao makuu washtakiwa wote wakiwa watumishi wa umma waliisababishia hasara NSSF kiasi cha zaidi ya Sh2 bilioni kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi.



Katika staka la tano tarehe hiyo hiyo katika ofisi za NSSF makao makuu ya NSSF washtakiwa wote kwa pamoja walijihusisha na  miamala haramu ya zaidi ya Sh2 bilioni huku wakifahamu fedha hizo ni mazalio ya kosa tangulizi.



Simon alidai upelelezi bado haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine.



Hakimu Mhina alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo isipokuwa  mahakama kuu pekee. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 15 mwaka huu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527