UZALISHAJI MAKAA YA MAWE WAONGEZEKA NCHINI | MALUNDE 1 BLOG

Tuesday, October 29, 2019

UZALISHAJI MAKAA YA MAWE WAONGEZEKA NCHINI

  Malunde       Tuesday, October 29, 2019
Na Asteria Muhozya

Imeelezwa kuwa, wastani wa uzalishaji wa Makaa wa Mawe nchini umekuwa ukiongezeka tofauti na ilivyokuwa  awali huku sababu kadhaa zikichangia ongezeko la uzalishaji huo ikiwemo mazingira mazuri ya uwekezaji, zuio la  Serikali kuingiza makaa ya mawe kutoka nje, ongezeko la viwanda vinavyotumia makaa ya mawe na  kuboreshwa kwa mundombinu ya usafirishaji. 


Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa wakati akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu  hatua zilizofikiwa katika  uendelezaji wa miradi ya makaa ya mawe kwa niaba ya Waziri wa Madini.

Mhandisi Mulabwa amesema katika kipindi cha miaka 8 kuanzia mwaka 2011 hadi 2018, uzalishaji uliongezeka kutoka tani 81,384.67 mwaka 2011 na kufikia  627, 651.00 mwaka 2018, ikiwa ni  wastani wa takribani tani 52,304.25 kwa mwezi.

‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miezi 9 kwa mwaka 2019, uzalishaji  uliongezeka  hadi kufikia tani 543,621.39 ikiwa ni wastani wa tani 60,402.38 kwa mwezi,’’ amesema Mhandisi Mulabwa.

Ameongeza kuwa, pamoja na ongezeko la uzalishaji huo, bado ni mdogo ikilinganishwa na kiasi cha makaa ya mawe kinachokadiriwa kuwepo nchini. Amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na mashapo ya makaa ya mawe  yanayofikia tani bilioni 1.9 na yaliyothibitishwa ni tani bilioni 1.4 huku ikitajwa kuwa nchi yenye akiba kubwa ya makaa hayo  kwa nchi za Afrika Mashariki.

‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti akiba kubwa zaidi kwa sasa inapatikana katika bonde la Mchuchuma ambapo kuna akiba ya zaidi ya tani milioni 400,’’ amesema Mhandisi Mulabwa.

Akizungumzia  mwenendo wa mauzo amesema kipindi cha kuanzia  mwezi Julai, 2018 hadi  Juni, 2019 kiasi cha makaa ya mawe kilichozalishwa na kuuzwa  ni tani 799,628.41 zenye thamani ya shilingi 102,922,127,876.61. Ameongeza kati ya kiasi hicho kilichozalishwa, tani 421,400.07 ziliuzwa nchini na tani 378,2228.34 ziliuzwa katika masoko ya  nje ya nchi

Ameeleza kutokana na mauzo hayo, Serikali ilipata kiasi cha  shilingi 4, 116,885, 115.06 , ambapo shilingi 3,087,663,836. 30 ni mapato yatokanayo na mrabaha na  shilingi 1,029,221,278.77 ni mapato yatkanayo na ada ya ukaguzi.kipindi cha kuanzia mwezi Julai.

Kuhusu uzalishaji wa makaa ya mawe kwa mwaka wa fedha 2019/20, kuanzia mwezi Julai 2019 hadi Septemba 2019 amesema  kiasi kilichozalishwa katika migodi yote ni tani 157,341 zenye thamani ya shilingi 16,691,662,474. 

‘’ Mhe. Mwenyekiti kutokana na mauzo hayo serikali ilikusanya mapato ya shilingi 949,834,017.71 ambapo shilingi  807,074,032.73 ni mapato yatokanayo na malipo ya mrabaha na shilingi 142,759,984.98 ni mapato yaliyotokana na ada ya ukaguzi.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na serikali kuendeleza miradi ya makaa ya mawe amesema kuwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha uanzishwaji wa Viwanda mbalimbali ili kujenga uchumi wa viwanda; kuendelea kusimamia tafiti maeneo mbalimbali ili kupata taarifa sahihi za kiasi cha mashapo na ubora wa makaa ya mawe nchini; wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara katika sekta ya makaa ya mawe; serikali imeendelea kufuatilia uanzishwaji wa miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga na kuendelea kuweka zuio la uingizwaji   wa makaa ya mawe kutoka nje ya nchi ili kuongeza biashara ya makaa ya mawe yanayozalishwa nchini.

Aidha, ameyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kuongeza kwa matumizi ya makaa ya mawe yanayozalishwa nchini kufuatia zuio la uingizaji wa makaa ya mawe kutoka nje,  kuongezeka kwa kiasi cha makaa ya mawe yanayozalishwa hapa nchini kutoka wastani wa tani 81,384.67 kwa mwaka 2011 hadi kufikia tani 627,651.00 mwaka 2018 kutokana na ongezeko la watumiaji wa ndani.

Pia, ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na  kuongezeka kwa biashara ya makaa ya mawe ndani  na nje ya nchi, ambapo watumiaji wa nishati ya makaa ya mawe wameendelea kuongezeka kutokana na upatikanaji wake, kuongezeka kwa mapato ya serikali kutokana na uuzaji wa makaa ya mawe na kuongezeka kwa ajira kutokana na shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe ambapo hadi kufikia Septemba 2019, takribani watu 500 wameajiriwa katika migodi mbalimbali  ya uchimbaji wa makaa ya mawe.

Kwa upande wa Kamati ya Bunge baada ya kupkea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula imeitaka wizara kuweka msukumo mkubwa wa uanzishwaji wa miradi ya Linganga na Mchuchuma pamoja na mradi wa Kiwira kutokana na manufaa yake kiuchumi. 

Akijbu hatua zilizochukuliwa na wizara, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema tayari wizara kwa upande wake imekwishafanya masuala yote yanayohitaji msukumo wa wizara katika miradi husika huku mengine yakisimamiwa na mamlaka nyingine hata hivyo ameeleza kuwa serikali inaendelea kuyafanyia kazi ili kuwezesha miradi hiyo kutekelezwa.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameileza Kamati hiyo kuhusu hatua kadhaa zilizochukuliwa na wizara katika kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya uchimbaji wa makaa ikiwemo ya kilomita 8 kutoka Kiwira mpaka Kabulo na kueleza kuwa, tayari serikali imekwisha tenga shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa daraja. 

Vikao kati ya  Kamati, Wizara na taasisi zake vimeanza Oktoba 28, 2019 na vinatarajiwa kuhitimishwa Novemba 1,2019.


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post