Picha : WANAWAKE WATIA NIA WAPEWA MAFUNZO KUGOMBEA NA KUSHINDA KWENYE UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA



Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Theresia Sawaya akizungumza katika mafunzo ya uongozi kwa wanawake watia nia ya kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kutoka vitongoji na vijiji kwenye baadhi ya kata wilaya Kishapu mkoani Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtandao wa Jinsia Tanzania 'TGNP Mtandao' umetoa mafunzo ya uongozi kwa Wanawake,vijana na watu wenye ulemavu waliotia nia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi  kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24,2019 ili kuwajengea uwezo,ujasiri,mbinu na mikakati ya kuingia katika kinyang'anyiro cha uchaguzi na kushinda.



Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Jumatano Oktoba 23,2019 kwenye ukumbi wa BM uliopo katika kata ya Maganzo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na kukutanisha watia nia 65 kutoka baadhi ya kata za wilaya ya Kishapu.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo,Theresia Sawaya ambaye ni Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wanawake,vijana na watu wenye ulemavu waliotia nia kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili waweze kugombea na kushinda kwa kishindo.

"Tumekutana na watia ni kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi ili kuwafundisha kuhusu dhana za jinsia na namna zinavyotumika na athari zake katika masuala ya uongozi lakini pia kuwajengea uwezo namna ya kufanya kampeni kwenye uchaguzi,namna ya kupata rasilimali fedha na ulinzi na usalama wa wagombea",alieleza Sawaya.

Alisema kupitia mafunzo hayo wanatarajia wanawake ambao katika miaka ya nyuma wamekuwa nyuma kushiriki kwenye masuala ya uchaguzi watahamasisha na kupata ujasiri wa kugombea na kushinda katika uchaguzi na kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Kwa upande wake, Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Eva Hawa ambaye pia ni mwezeshaji katika mafunzo hayo aliwataka wanawake watia nia kugombea kwenye uchaguzi kuhakikisha wanawashirikisha waume zao ili kupata matokeo mazuri zaidi.

"Wanawake tunapogombea madaraka ni vyema kuwashirikisha watu wanaotuzunguka,washawishini waume zenu wawaunge mkono ikibidi muwaombe wawe makampeni meneja wenu,wataongea na wanaume wenzao ili wawape kura na mtapata ushindi mnono",alisema Juma.

Aidha aliwataka wazazi kutowabagua watoto kwa kuwapa kipaumbele zaidi watoto wa kiume huku akisisitiza kuwa kama wazazi wawape majukumu sawa.

"Tuwafundishe watoto wa kiume kuacha kuwa tegemezi,tuwafundishe kushirikiana na dada zao kufanya kazi wanazopewa nyumbani,kwani mtoto wa kike siyo mfanyakazi wa nyumbani, mtoto wa kike anapaswa kupewa haki sawa na mtoto wa kiume",alisema.
Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Theresia Sawaya akielezea kuhusu mafunzo ya uongozi kwa wanawake watia nia ya kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kutoka vitongoji na vijiji kwenye baadhi ya kata wilaya Kishapu mkoani Shinyanga.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Theresia Sawaya ambaye ni Mwezeshaji katika mafunzo ya uongozi kwa wanawake watia nia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa akiwahamasisha wanawake kujiamini kwani wanaweza kuongoza jamii kutokana na kwamba mwanamke ni kiongozi kuanzia ngazi ya familia.

Wanawake watia nia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wakiwa ukumbini. 

Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Eva Hawa ambaye pia ni mwezeshaji katika mafunzo ya uongozi kwa wanawake watia nia kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa akiwasisitiza kuepuka rushwa ya ngono kwenye uchaguzi.
Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Eva Hawa akizungumza wakati wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake watia nia kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa akiwasisitiza kuepuka rushwa ya ngono kwenye uchaguzi.
Diwani wa Kata ya Mwadui Luhumbo,Mhe. Sarah Masinga akiwatia moyo wanawake waliotia nia kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa wajiamini,wamtangulize Mungu na kushirikiana na jamii ili kushinda katika nafasi wanazogombea.
Washiriki wa mafunzo hayo wakisiliza nasaha mbalimbali.


Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu Rahel Madundo akiwasisitiza wanawake kupendana na kuacha tabia ya kukwamishana wao kwa wao.
Mtia nia ya kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,Mary Richard Nzingula akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Mlezi wa wanawake watia nia ya kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wilaya ya Kishapu,Mhe. Suzana Makoye ambaye ni Diwani wa Viti Maalum kata ya Maganzo akiwasisitiza wanawake watia nia kutokata tamaa pale wanapokutana na changamoto mbalimbali.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Soma Pia : MWANASHERIA TGNP MTANDAO : WANAWAKE MSIKUBALI KUTUMIA MIILI YENU KUWEZESHWA KISIASA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527