RC MAKONDA AWATAKA TBA KUKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA HALMASHAURI YA UBUNGO KABLA YA DISEMBA 30


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amewataka Wakala wa Majengo Tanzania TBA kuhakikisha ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo unakamilika na kuanza kutumika kabla ya Disemba 30 Mwaka huu likiwa Viwango na Ubora unaotakiwa.

Makonda ameeleza kuchukizwa kuona mkataba wa ujenzi huo umesainiwa tangu Disemba 13 mwaka jana na kazi inatakiwa kukamilika Disemba 13 mwaka huu lakini hadi sasa ujenzi umefikia 35% huku muda wa mkandarasi kuwa site ukiwa mkubwa kuliko kazi aliyoifanya.

Makonda amebaini kuwa ujenzi ulisimama kwa zaidi ya Miezi miwili kwa kigezo cha Manispaa kuchelewa kutoa fedha huku muhusika akikaa kimya pasipo kutoa taarifa kwenye ngazi ya Mkoa ili mkoa uweze kuingilia kati fedha itoke kwa wakati.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya Ujenzi wa Daraja la Kisasa la Juu (Interchange) Ubungo ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo na kumuelekeza mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Pamoja na hayo Makonda pia amefanya ziara ya Ukaguzi wa Maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha na kueleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

Katika ziara hiyo Makonda ametembelea Ujenzi wa Kituo cha Afya Kimara na kumuelekeza Katibu tawala wa Mkoa huo kutuma timu ya kufuatilia upya ujenzi wa Jengo la gorofa katika kituo hicho linalogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 baada ya kubaini gharama za ujenzi ni kubwa kuliko idadi ya majengo wakati Wilaya ya Kigamboni imetumia Bilioni 1.5 kujenga majengo saba ya kisasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527