TANZANIA KUPOKEA WATALII ZAIDI YA 1000 KUTOKA NCHINI ISRAEL


Tanzania inatarajia kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka nchini Israel ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii mwezi huu wa Oktoba.

Kundi la kwanza lililokuwa na zaidi ya watalii 200 liliwasili nchini kuanzia tarehe 05 Oktoba na kundi la pili lenye zaidi ya watalii 520 linatarajiwa kuwasili nchini tarehe 12 na kundi la tatu lenye watalii zaidi ya 200 litawasili nchini tarehe 13 Oktoba kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Watalii wengine zaidi wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu baada ya Makampuni ya Uwakala wa Utalii kukamilisha taratibu za safari zao.

Watalii hao wanatarajiwa kutembelea Visiwa vya Zanzibar, Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangire na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Ujio wa watalii hao unatokana na jitihada za kuitangaza nchi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na wadau wa utalii  wa ndani na nje ya nchi.

Tanzania imejipanga kuwapokea na kuwatembeza watalii hao katika vivutio vya utalii vilivyoko nchini. Serikali inawakaribisha watalii hao kutembelea vivutio hivyo vya utalii ambavyo nchi imebarikiwa kuwa navyo ili wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania nchini kwao na kwingine watakakokwenda.

Imetolewa na:Dkt. Faraji K. Mnyepe

Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
DODOMA


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527