KIKWETE AKERWA NA WANAOTAFSIRI VIBAYA HOTUBA YAKE

Ofisi ya Rais mstaafu wa awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, imewataka baadhi ya watu kuacha kutoa tafsiri isiyo sahihi, kuhusu alichokizungumza katika kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere. 

Taarifa hiyo iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Oktoba 11, imeeleza masikitiko yake kuhusu upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu, kuhusu hotuba aliyoitoa Oktoba 8, 2019, katika Kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kivukoni.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika kongamano hilo Rais Mstaafu, alieleza namna alivyokuwa akimfahamu Hayati Baba wa Taifa, lakini kilichowashangaza ni kujitokeza kwa baadhi ya watu wachache wanaopotosha ukweli kuhusu maneno aliyoyasema kwa kujaribu kuweka maneno ambayo hakuyatamka kinywani mwake kwa madai ya kuwa anawasema baadhi ya viongozi waliopo sasa.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, Dkt Kikwete, hakufanya ulinganifu wowote kati ya Mwalimu Nyerere na marais waliopo na waliomaliza muda wao na kwamba huo ni uzandiki, fitna na uchonganishi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527