MABULA ALITAKA SHIRIKA LA NYUMBA KUJENGA MAJENGO YENYE UBORA

Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha linajenga majengo yenye ubora katika miradi mbalimbali inayopewa kujenga nchini.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Kanda ya Ziwa (TFS) eneo la Mkolani jijini Mwanza akiwa katika ziara yake ya kuangalia utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika Kanda ya Ziwa pamoja na kukagua miradi ya ujenzi inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

Alisema ni vyema shirika hilo likahakikisha miradi yoyte inayopewa ya ujenzi inakuwa na viwango na kuepuka udanganyifu wowote unaoweza kufanyika kama vile kuweka kiwanga kidogo cha saruji katika ujenzi jambo linaloweza kusababisha majengo yasiyo na ubora.

Aliwataka wafanyakazi wa mradi wa ujenzi wa jengo la TFS mkoani Mwanza kuwa waaminifu wakati wote wa ujenzi ili kuepuka sifa mbaya ya udokozi inayoweza kusababisha shirika la Nyumba kukosa kazi nyingine kwa kujenga majengo yaliyo chini ya kiwango.

‘’Uaminifu lazima uwepo ili ikitokea kazi nyingine mpewe awamu hii NHC mko vizuri’’ alisema Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alilisifu shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kufanya kazi vizuri katika ujenzi wa Ofisi na nyumba za watumishi na kulitaka shirika hilo kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa majengo yake katika kipindi kifupi kwa kuwa linahitaji kufanya kazi usiku na mchana.

Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mwanza Fadhili Ntahena alisema, ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Ziwa unaosimamiwa na shirika lake unagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 na ulianza Septemba mwaka huu ikiwa ni sehemu ya miradi mbalimbali ambaloShirika hilo limepewa na serikali kuijenga.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ubunifu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Magreth Ezekiel alisema, NHC imejipanga katika miradi yake mbalimbali iliyokabidhiwa na mipango ya Shirika ni kuhakikisha miradi yote inakamilika ndani ya miezi sita na mradi wa ujenzi wa jengo la TFS Mkolani Mwanza walipanga kumaliza April 2020 ingawa jengo hilo linaweza kukamilika kabla ya mwezi huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527